CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) kimemuenzi Mwalimu Julius Nyerere kwa kufanya kikao maalumu
cha Kamati Kuu ya chama hicho na kuomba wajumbe wake kutambua umuhimu wa
siku hiyo.
Akifungua kikao hicho cha siku mbili,
kinachofanyika kuanzia Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe alisema wanatambua umuhimu wa kumbukumbu ya kifo cha Baba
wa Taifa Mwalimu Nyerere hivyo wamefanya mkutano huo ili kuenzi mambo
aliyoyafanya kwa ajili ya taifa.
“Leo ni kumbukumbu ya miaka 15 ya kifo
cha Baba wa Taifa Nyerere, tunatambua umuhimu wa siku hii na tulipanga
kwa makusudi siku hii tufanye kikao kwa kumuenzi baba yetu aliyefanya
makubwa kwa manufaa ya Tanzania,” alisema Mbowe.
Alisema katika kumuenzi Mwalimu Nyerere
wajumbe hao watakumbuka kuwa mwaka 1995 enzi za uhai wake, Mwalimu
alizungumza na Watanzania na kuwaambia ikiwa wanataka mabadiliko
wanaweza yapata ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), au nje ya chama
hicho.
Aliongeza kuwa, kwa hali ilivyo wananchi
wanahitaji mabadiliko na kwamba mchakato wa katiba ulikuwa njia mzuri
ya kuanzisha mabadiliko hayo, lakini akadai mchakato mzima umevurugwa na
hakuna dhamira ya mabadiliko ya kweli.
Kuhusu suala la daftari la kupiga kura,
Mbowe alisema daftari hilo linapaswa kuboreshwa kwa kuwa kuna idadi
kubwa ya wananchi hawakuandikishwa, hivyo kwenye uchaguzi mkuu ujao
watakosa haki yao ya kupiga kura.
Pamoja na mambo mengine, kikao hicho pia
kilijadili agenda mbalimbali 11 na kufanya uteuzi wa bodi ya wadhamini
wa chama hicho, kufanya uteuzi wa makatibu wa wilaya na mikoa na
kujadili mapendekezo ya katiba pamoja na kupokea taarifa ya ukaguzi wa
hesabu za chama hicho.