MFANYABIASHARA wa Arusha anayemiliki kampuni ya Tanzania Bush Camp
yenye kambi za watalii katika hifadhi za Serengeti mkoani Mara na
Manyara iliyopo katika mikoa ya Arusha na Manyara, Timoth Mroki (36)
amejiua kwa kujipiga risasi tatu kifuani akiwa katika baa maarufu ya
Arusha Raha iliyopo eneo la Shams, jijini hapa.
Kisa cha kujiua kwake kimetajwa ni kusababisha ajali, baada ya
kuligonga gari lingine katika eneo la Mbauda wakati akitoka katika
makazi yake yaliyopo eneo la Kwa Mrombo, jijini hapa.
Alifikwa na mauti katika tukio lililotokea kati ya saa 1:30 na saa 2:00 usiku, ndani ya baa hiyo.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, Mroki alifika katika baa hiyo
baada ya kufanikiwa kuwatishia kwa risasi waendesha bodaboda waliokuwa
wamemzingira katika eneo la ajali na kisha kuondoka kwa kasi kwa gari
lake aina ya Nissan Navara.
“Alipiga risasi mbili hewani waliokuwa wamemzunguka wakanywea,
akatumia mwanya huo kukimbia na moja kwa moja akafika Arusha Raha
pengine kwa lengo la kujificha, na hapo akaanza kunywa…
“Ingawa inaonekana alikotoka alikunywa kidogo, alipofika Arusha Raha
alikunywa haraka pombe mbili kali aina ya Valuu (Valeur) na wakati
anamalizia ya tatu, akajikuta anazingirwa tena na wale waendesha
bodaboda,” anasema mtoa habari huyo na kuongeza kuwa, baada ya kufyatua
tena risasi mbili nyingine hewani, lakini bila ya dalili ya watu hao
kutishika, ndipo akaamua kujimiminia risasi.
Habari zaidi zinasema wakati anazingirwa, naye akijihami kwa risasi
wasamaria wakiwa katika harakati za kupiga simu Polisi walishtukia
wakiingia katika eneo la tukio lakini tayari Mroki alikuwa ameshajitoa
uhai baada ya kujimiminia risasi kifuani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatusa Sabas hakupatikana
kuzungumzia tukio hilo, ingawa Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi ya wilaya ya
Arusha imekiri kuwepo kwa tukio hilo, lakini chanzo chetu kikikataa
kutajwa jina gazetini kwa kuwa si wasemaji wa matukio ya polisi mkoani
Arusha.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru.
Na John Mhala, Arusha