Madereva wa Kampuni ya Usafi jijini Dar es Salaam (UDA), leo wamegoma
kuingiza mabasi barabarani kwa kinachoelezwa ni madai mbalimbali ya
haki zao dhidi ya shirika hilo.
Kwa mujibu wa dereva mmoja ambaye hakupenda kuweka wazi jina lake,
wamefikia hatua hiyo kufuatia uongozi wao kutosikia kilio chao cha
kupunguziwa kiasi cha fedha wanachotakiwa kukipeleka kwa siku.
Dereva huyo alisema kuwa, hesabu wanayotakiwa kupeleka ni shilingi 205000 kwa njia zote ambayo ni nyingi sana.
Aliongeza licha ya kuuomba uongozi upunguze kiasi hicho hadi kufikia
shilingi 160,000 wamegoma, pia wamekuwa wakicheleweshewa mishahara
ambapo mshahara wa mwezi uliopita hawajalipwa hadi leo, kutowekewa fedha
za NSSF.
Dereva huyo aliongeza kuwa kero nyingine ni pale inapotokea
wamekamatwa kwa makosa ya barabarani na kuwekwa mahabusu, wao huyafuata
magari yao tu na kuwaacha wao wakisota ndani.
Madereva hao wanaomba kukutana na uongozi wa juu wa shirika hilo ili kukaa na kuzungumza nao kwa lengo la kufikia muafaka.
Mgomo huo umeleta usumbufu kwa wakazi wengi wa jiji hususan wa
Mbagala ambapo wafanyakazi wengi leo wamechelewa kufika maofisini na
kwenye shughuli zao zinazowapatia kipato.
Na Kulwa Mwaibale