NA KENNETH NGELESI,EDDY BLOG NJOMBE
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Anglikana
Tanzania, Jackobo Chimeledya, amesema katiba haitakuwa na faida kwa watanzania,
iwapo wananchi hawataelimishwa na kupewa muda wa kutosha kabla ya kupiga
kura ya maoni.
Rai hiyo ilitolewa hivi
karibuni na Askofu huyo mkoani
hapa, wakati wa ibada ya kumuweka Wakfu Askofu Mathew Mhagama, kuwa
Askofu wa Nane wa Jimbo la Kusini Magharibi Tanganyika ,katika kanisa kuu
la Mtakatifu Andrea Mjini Njombe.
Alisema kuwa kwa kuwa katiba hii
haiwezi kutumika kwenye uchaguzi mkuu ujao alishauri kuwa na
muda mrefu wa kutoa elimu kwa wananchi kabla ya kuanza zoezi la kura ya
maoni ili, kila mmoja awe na uelewa wa kupiga kura ya ndiyo ama hapana.
“ Ingekuwa ni amri yangu ningependa
wananchi wapewe elimu ya kutosha hata ikibidi kuanzia miaka miwili hadi mitatu,
ili wajue na wawe na ufahamu wa kutosha, na hiyo itasaidia kufanya maamuzi
sahihi yakura ya ndio ama hapana ya katiba.
Aidha Askofu Chimeledya pia
aliwataka viongozi wote wakiwemo wa dini,serikali na siasa kuheshimu mawazo ya
wananchi, na kuwataka viongozi kuzingatia maadili, na kudai kuwa ikiwa
kipengele cha maadili ya viongozi kitaondolewa kwenye katiba, kutakuwa na
mapungufu mengi kwenye utendajikazi.
“ Katiba ni msingi wa kuleta maisha
bora kwa kila mtanzania ni bora kama kunavitu vya kubadili,vibadilike
kwamanufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla hata kama ni miaka mitano ili mradi
tuwe na kitu kizuri” Alisema Askofu huyo.
Naye Waziri wa Maliasili na Utalii
Lazaro Nyalandu, aliyekuwa mgeni rasmi kwenye ibada hiyo, akimuwakilisha waziri
Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Pinda ,alisema jamuhuri
itaendelea kuheshimu uhuru wa kuabudu.
Waziri Nyalandu aliwahakikishia
viongozi wa dini kuwa serikali ya Jamuhuri ya Muungano itaendelea kutoa uhuru
wa kuabudu kwa dini zote huku akiwataka viongozi wa dini kuhakikisha
wanawasaidia vijana ambao ni taifa la kesho kwa kuwalea kwenye maadili.
Hata hivyo serikali iliahidi
kuchangia shilingi milioni 50 kwenye mradi wa kupanda miti kwaajili ya utuzaji
wa mazingira,huku waziri huyo na familia yake wakiahidi shilingi milioni kumi
kwaajili ya kusaidia mfuko wa Akofu wa Jimbo hilo wa kusomesha watoto Yatima.