JESHI
la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limekanusha vikali uvumi unaoendelea
kuzushwa jijini Dar es Salaam kuhusu utekeaji nyara wa watoto wadogo wanaosoma
shule za jiji hilo na kuwataka wananchi kuupuuza.
Akizungmza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya
Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema kuwa mpaka sasa jeshi hilo halina taarifa
yoyote ya mtoto kutekwa au kufanyiwa madhara yoyote kwa mtindo wa utekaji
nyara.
“Jeshi
la Polisi limegundua kwamba huu ni uvumi ambao haujulikani chanzo chake hivyo
wananchi wanaombwa kuachana nao na kuupuza kwani unaleta hofu katika jamii bila
sababu za msingi” alisema Kova.
Alisema
kuwa pia uvumi huo umeanza kuleta usumbufu ambapo mnamo Oktoba 3 mwaka huu saa
3:00 asubuhi huko Vingunguti, mtu mmoja aitwaye Prosper Makame (34) akiwa na
mkewe Marystella Munis (30) walipata usumbufu unaotokana na uvumi huo.
Kamishna
Kova aliongeza kuwa watu hao ambao ni wafanyabiashara wa vyombo vya nyumbani
walifika maeneo ya shule ya msingi Kombo iliyopo Vingunguti kwa ajili ya
biashara zao, wakiwa na gari aina ya Noah yenye namba T252 DAY, ghafla walizingirwa na watu
wakidaiwa wanateka wanafunzi.
“Pia
mnamo Oktoba 13, 2014 majira ya saa 4:00 asubuhi huko katika kituo cha Polisi
Tabata uliibuka uvumi kuwa gari namba T548 BUN aina ya Noah rangi nyeusi ambayo
ni mali ya askari polisi A/INSP Ester wa kikosi cha usalama barabarani,
ilivumishwa kwamba ndani ya gari hiyo kuna vichwa vitano vya watoto wa shule ya
msingi Mtambani na kusababisha wazazi wenye watoto wanaosoma shule hiyo
kukusanyika kituoni hapo ili kushuhudia na kuona vichwa hivyo” alisema Kamishna
Kova na kuongeza:
“Na
ndipo Mkuu wa kituo hicho cha Polisi
aliamuru gari hilo lifunguliwe na kuwathibitishia wananchi kuwa habari hizo ni
za uongo na uvumi”
Kutokana
na tukio hilo jeshi hilo lilifanya uchunguzi na kumkamata mtu mmoja Gilbert
Stanley (32) mhehe mkulima na mkazi wa Tabata alipohojiwa alikiri kueneza
habari hizo na kudai yeye aliambiwa na mtu ambaye hakumkumbuka.
Hivyo,
Kamishna Kova alisisitiza kuwa uvumi wa kuwepo kwa kikundi cha wahalifu
wanaowateka watoto wanafunzi si wa kweli hata kidogo na hivyo wananchi
wanatakiwa kuepukana na taarifa hizo kwani zinaweza kusababisha uvunjifu wa
amani.
Katika
hatua nyingine,
Kamishna Kova alithibitisha kutokea kwa vifo vya watu watano na wengine 16
kujeruhiwa katika ajali ya moto iliyotokea Oktoba 13 mwaka huu majira ya saa
5:00 usiku huko kwenye mzunguko wa Mbagala Charambe baada ya lori aina ya
Scania T347 BXG lilipoanguka likiwa na
mafuta aina ya petrol lita 38,000.
Aliwataja
waliofariki kuwa ni Masoud Masoud mkazi wa Charambe, Hassani Mohamed mkazi wa
Mbagala Kibangulile, Mohamed Ismail, Ramadhani Halfan na Maulidi Rajabu wote ni
wakazi wa Mbagala Charambe.
Alisema
kuwa majeruhi wamelazwa kwenye hospitali ya taifa ya Muhimbili na hospitali ya
wilaya ya Temeke wakiendelea na matibabu huku ajali hiyo pia ikisababisha
nyumba ya kulala wageni iitwayo United kuungua moto na kuteketea kwa pikipiki
saba za bodaboda zilizokuwa zimeegeshwa karibu na aneo hilo, maduka matano
yenye bidhaa zenye thamani ya shilingi Milioni 197 yaliungua moto.
Kamishna
Kova aliwataka wananchi kuacha tabia ya kukimbilia kwenye ajali za magari ya
mafuta kwani ni hatari kwa maisha yao kwani watu wengi waliojeruhiwa walikuwa
wakichota mafuta yaliyomwagika kutokanana ajali hiyo.
Katika
tukio lingine,
Kamishna Kova alisema kuwa Jeshi hilo limefanikiwa kumkamata jambazi sugu
aitwaye Paulo Thamas Milanzi maarufu Chinga
(35) mmakonde mkazi wa Chanika
ambaye baada ya majibizano ya risasi jambazi hilo lilijeruhiwa na kufikshwa
hospitali ya muhimbili kwa matibabu ingawa baadaye alifariki dunia.
Alisema
jambazi hilo lilikuwa likitafutwa na polisi kutokan na kuhusika kwenye matuio
ya mauaji na wizi ikiwemo tukio la kuuawa kwa Afisa Mwandamizi wa Usalama wa
Taifa, Sylivabus Adrian Mzeru Aprili 29 mwaka huu liliotokea Uwanja wa Ndege.
Aliongeza
kuwa jambazi lilikamatwa na bastola aina ya Star ambapo majambazi wenzake
walikamatwa na sasa wako gerezani, hivyo ameitahadharisha jamii iachane na
uhalifu kwani hauna manufaa yoyote.