MWANAMKE Mkenya amezuiliwa kwa wiki tatu bila chakula katika nyumba moja nchini Saudi Arabia ambako ameajiriwa kama kijakazi.
Bi Anne Njeri
Mwaura, mwenye umri wa miaka 27, alitarajia kupata kazi ambayo
ingemsaidia kuwalea wanawe wawili aliowaacha nyumbani kwao Limuru,
Kaunti ya Kiambu.
Lakini sasa anahangaika nchini Saudi Arabia anaomba asaidiwe kurudi nchini akisema maisha yake huko yamegauka mateso.
Akisimulia Taifa Leo
masaibu yake kwa simu Jumatano, Njeri alisema amekuwa akinywa maziwa ya
mtoto au kula makombo kutoka kwa pipa la takataka kwa sababu mwajiri
wake wanamnyima chakula.
“Mwajiri
wangu aliniambia hakuna chakula changu kwa sababu alininunua kwa pesa
nyingi sana. Hapa nyumbani hawapiki. Wanalala mchana kutwa kisha usiku
wanatoka. Sijala, naumia, nateseka, sijaona uzuri wowote wa kuishi
huku,” akaeleza mwanamke huyo huku akilia.
Njeri anasema kuwa akitoka Kenya ajenti aliyedhamini ziara yake alimwambia ataajiriwa mjini lakini anakoishi sasa mashambani.
“Niko katika
eneo la Quriyat, karibu na mpaka wa Saudi Arabia na Jordan. Nikiondoka
Kenya niliambiwa nitaajiriwa mjini Dammam lakini kutoka hapa kwenda huko
inachukua saa 21,” akaeleza.
“Kazi ni
ngumu na nyingi sasa; Njaa ni nyingi. Mungu ndiye anajua ninayopitia.
Najihisi mdhaifu sana, naomba tu nirudi Kenya nikiwa mzima,” akasema.
Njeri pia
alituma video ambapo amejirekodi akiomba Wakenya wamsaidie kwa kuwa
ajenti aliyemsaidia kwenda huko amekataa kuwasiliana naye.
“Mara mwisho
kuongea naye (ajenti) nilikuwa katika Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta,
Nairobi. Nimejaribu kuwasiliana naye lakini amekataa kuzungumza nami,”
anasema Njeri katika video hiyo.
Anasema alinyang’anywa paspoti yake na mwajiri wake punde tu baada ya kuwasili nchini humo.
“Sina
pasipoti, walichukua. Ajenti wangu ndiye anaweza kunirudisha nchini
nikiwa salama kwa sababu anajua kila kitu,” anasema Bi Njeri.
Ajenti wake, Bi Eva Kambo, aliambia Taifa Leo kesi hiyo inaendelea kushughulikiwa.
Kurudi kenya
“Tulikuwa tukingoja afisi za ubalozi Saudi Arabia zifunguliwe. Anashughulikiwa na atarudi nchini haraka iwezekanavyo,” akasema.
Bi Kambo
alionya kuna baadhi ya matapeli wanaodai Sh300,000 ndipo Bi Njeri
aachiliwe na kuongeza kuwa hakuna pesa zozote zinazofaa kutolewa.
Lakini Bi
Njeri haamini anayosema ajenti wake akisema anajua visa vingi vya
wafanyakazi wanaoteseka katika nchi za Uarabuni huku maajenti wao
wakinyamaza.
“Simwamini
kamwe. Aliniambia naenda Dammam lakini sasa natesekea huku mashambani
bila hata chakula. Usalama wangu umo mikononi mwa Mungu sasa,” anasema
Njeri.
Mumewe Njeri,
Bw Michael Muiru, ambaye mwanzoni alipinga safari yake Uarabuni,
aliambia 'Taifa Leo’ anaamini uamuzi wa mkewe ulitokana na kushinikizwa
na marafiki wanaofanya kazi huko.
“Hatuna
mapato makubwa lakini sikutaka aende. Namhurumia sana, naomba tu
asaidiwe arudi nyumbani. Siwezi kumpuuza wakati kama huu,” akasema.
Wizara ya
Masuala ya Kigeni nchini imeahidi kushirikiana na ajenti huyo
kuhakikisha Njeri amerudishwa nchini salama haraka iwezekanavyo.