Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai(DCI), Isaya Mungulu amesema jalada la upelelezi wa kesi ya mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe limeshakabidhiwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kwa ajili ya kumfikisha mahakamani.
DCI Mungulu alisema hayo jana alipozungumzia
mwafaka wa shauri la mwenyekiti huyo aliyetangaza maandamano ya amani
kwa wafuasi wa chama chake mara baada ya kuchaguliwa tena kukiongoza kwa
miaka mitano mingine.
Alisema DPP ndiye mwenye uamuzi wa lini Mbowe atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
“Sisi tulishakamilisha taratibu zinazotuhusu na
tayari tumeshapeleka jalada kwa DPP. Yeye ndiye mwenye mamlaka ya kuamua
lini kesi hiyo itafikishwa mahakamani,” alisema.
Mbowe alitangaza maandamano hayo ya amani nchi
nzima mara tu alipochaguliwa kuiongoza Chadema kwa msimu wa tatu, mapema
Septemba mwaka huu katika siku aliyotimiza miaka 53 ya kuzaliwa kwake.
Baada ya kutoa tamko hilo, Jeshi la Polisi
lilimwita kumhoji kwa zaidi ya saa nne kwa madai kuwa kauli yake ilikuwa
na mlengo wa kichochezi.
Aidha, polisi walilazimika kutumia mabomu ya
machozi kuwatawanya wafuasi waliomsindikiza mwenyekiti huyo makao makuu
ya jeshi hilo.
Kutokana na tamko hilo la mwenyekiti, wafuasi wa
chama hicho waliendesha maandamano katika mikoa mbalimbali na kuwapa
polisi wakati mgumu kuyadhibiti kutokana na kutoyatambua kisheria.
Kuhusu utekelezaji wa tamko la mwenyekiti huyo,
Mngulu alisema kuwa jeshi lake linaendelea na taratibu za kuwafikisha
mahakamani makada wote waliokataa kutii amri halali iliyotolewa kuwaonya
kuhusu maandamano hayo.
“Licha ya kwamba tulitoa angalizo hilo, lakini
wengi walikaidi amri yetu, japokuwa tulijitahidi na kuyazima. Wapo watu
kadhaa tunawashikilia katika mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Mtwara,
Dodoma na Mara. Hatua za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi yao,”
alisema.