CHADEMA WAPINGA MWANASHERIA MKUU WA ZANZIBAR KUFUTWA KAZI

Chama cha  Demokrasia  na  Maendeleo  (Chadema)  kimesema hakijafurahishwa  na  kitendo kilichofanywa na Rais wa Zanzibar. Dk. Ali Mohammed Shein, cha  kumfukuza  Mwanasheria Mkuu  wa Zanzibar, Othman Masoud.
Akizungumza  na  wanachama wa Chadema, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Salum Mwalimu,  alisema  kitendo  cha  kuvuliwa  uanasheria mkuu Othman, kinadhihirisha kuwa Rais Shein yupo kichama zaidi na siyo kutetea maslahi ya Zanzibar.

Alisema kitendo  kilichofanywa na Othman katika Bunge Maalumu la Katiba kwa kukataa baadhi ya vifungu  vya katiba inayopendekezwa ni cha ushujaa  na  ujasiri  katika kupigania maslahi ya Wazanzibari na ana imani  kuwa  uamuzi  wake huo ndiyo uliosababisha avuliwe wadhifa aliokuwa nao.

Alisema kilichobaki kwa wananchi ni kuikataa katiba iliyopitishwa na Bunge hilo kama serikali ya Zanzibar ilivyomkataa Othman.

“Chama tawala kilitaka kumtumia mwanasheria huyo kama kikaragosi na kutumikia maslahi ya chama hicho badala ya kuwatumikia wananchi. Lakini kwa kuwa mwanasheria huyo anajielewa, alishindwa kufanya hivyo,” alisema Mwalimu.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alisema matumaini ya chama chake ni kushirikiana na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ili kuhakikisha wanaing’oa CCM madarakani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

“Ukawa haijavunja vyama vya upinzani, bali upo katika utaratibu mzuri. Na tayari tumeshakubaliana vyama viendelee kujijenga ili viimarishe ushirikiano,” alisema Dk. Slaa.

Viongozi hao walipokelewa na wafuasi wao katika viwanja vya ndege vya Amani Abeid Karume kwa shangwe na nderemo hadi makao makuu ya Chadema, eneo la Darajabovu, ambako askari polisi walifika eneo hilo wakiwa kwenye magari aina ya Land Rover Defender wakibeba silaha na kuwaamuru wafuasi wa chama hicho watawanyike eneo hilo.

Chadema leo inatarajia kufanya mkutano wa hadhara katika viwanja vya kwa Mabata Amani, ambako Naibu Katibu Mkuu wake Tanzania Bara, John Mnyika, atahutubia.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo