Matukio ya kuuawa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino)
yamezuka upya mkoani Simiyu, baada ya Mughu Lugata (40) kuuawa kinyama
kwa kukatwakatwa mapanga na watu wasiojulikana huku wakitoweka na baadhi
ya viungo vyake.
Tukio hilo lililotokea Kitongoji cha Chalala,
Kijiji cha Gasuma, Kata ya Nkololo, wilayani Bariadi, mkoani hapa,
Lugata alikatwa mguu wake wa kushoto sehemu ya goti, vidole viwili vya
mkono wa kushoto kucha ya kidole gumba ambavyo wauaji walitoweka na vyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo alisema tukio hilo
lilitokea juzi saa 12:00 usiku nyumbani kwa Lugata.
“Lugata aliuawa na mguu wa kushoto kuchukuliwa kwa
kukatwa sehemu ya goti, vidole viwili vya mkono wa kushoto na kucha ya
kidole gumba cha mkono wa kushoto, wauaji waliondoka navyo,” alisema
Mkumbo.
Mkumbo alisema Lugata akiwa amelala peke yake
nyumbani kwake, alivamiwa na watu wasiojulikana na kuanza kumkatakata
mapanga na kuchukua baadhi ya viungo vyake vya mwili na kutokomea navyo
kusikojulikana.
Alisema tayari wanawashikilia watu wawili, mmoja ni mganga wa kinyeji mkulima wa kijiji hicho.
Mkumbo alisema mtuhumiwa mwingine alikuwa kwa
mganga huyo wakiwa na vifaa vya kupigia ramli na kwamba, chanzo cha
tukio hilo ni imani za ushirikina.
Aliwataka wananchi wenye taarifa juu ya wahusika
wa tukio hilo kusaidia polisi, ikiwamo kuacha kudanganyika kuwa utajiri
unakuja kwa imani za ushirikina, bali kufanya kazi kwa bidii.
Alisema kuna baadhi ya waganga wanawadanganya
wateja wao kuwa, viungo vya walemavu wa ngozi vinaleta utajiri hali
ambayo inawasababisha kuamini na kuendeleza mauaji ya albino.
Kasi ya mauaji dhidi ya albino ilikuwa imepungua
baada ya Serikali na mashirika ya ndani na nje kupiga vita mauaji hayo,
lakini tukio hili linaanza kutonesha vidonda na kuhatarisha usalama wa
walemavu hao.
Na Na Faustine Fabian
Na Na Faustine Fabian