WAZIRI CHIZA NUSURA ABUBUJIKWE NA MACHOZI KISA UFISADI MKOANI MBEYA


WAZIRI wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, nusura atokwe na machozi baada ya kukuta bwawa la umwagiliaji lililojengwa kwa zaidi ya sh. bilioni 3 limebomoka.
 
Hali hiyo ilimfanya awaweke kitimoto wahandisi wa Ofisi ya Umwagiliaji Kanda ya Mbeya.
 
Alisema ujenzi wa bwawa hilo ambalo lilikuwa linatarajiwa kutumiwa na wananchi zaidi 6,000 umejaa harufu ya ufisadi, hivyo ataunda tume itakayochunguza zabuni ilivyotangazwa,uwezo wa mkandarasi, matumizi ya fedha na utaalamu uliotumika.
 
Alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha kila aliyehusika kutoka katika wizara yake, Ofisi ya Umwagiliaji Kanda ya Mbeya hasa wasimamizi ili kuhakikisha wanawajibishwa.
 
"Hapa tunazungumza habari za utaalamu nami kama mhandisi mwenzenu nawaambieni wazi kuwa hapa mmeniangusha na kunifedhehesha,kwani mmenipa wasiwasi mkubwa jinsi mlivyoteketeza mabilioni ya fedha za kodi za Watanzania ambayo yangetumika kuwasaidia wengi, sasa nasema nataka kupata taarifa kamili baada ya uchunguzi," alisema.
 
Alisema kuwa wakati zaidi ya bilioni tatu zimetumika bila mradi kukamilika anashangaa kusikia kuwa mkandarasi wa kampuni ya Boymanda iliyojenga wigo huo ikidai kuongezewa zaidi ya milioni 600 kwa ajili ya kumalizia kazi hiyo jambo ambalo ni wizi mkubwa wa fedha za Watanzania.
 
Chiza alisema amekerwa na majibu ya wahandisi wake na ushirikiano uliokuwepo na wahandisi wa Halmashauri ya Mbarali. Alisema kazi ya Serikali lazima ifanywe kwa ushirikiano mkubwa bila ya kuwa na kificho.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo