JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limefanikiwa kumkamata Ofisa Usalama wa Taifa feki ambaye amekuwa akijipatia fedha kutoka kwa wafanyabiashara kwa kuwahusisha na makosa yanayohatarisha usalama wa nchi.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Kanda
Maalum ya Dar es Salaam; Kamishna Suleiman Kova, alimtaja ofisa huyo
feki kuwa ni Saimoni Meena (40) mkazi wa Tabata Kinyerezi jijini Dar es
Salaam.
Kova
alisema mtuhumiwa huyo pia anatuhumiwa kuwasumbua wafanyabiashara
mbalimbali jijini Dar es Salaam kwa kuwasingizia au kuwatuhumu kwamba
wanahusika na makosa yenye kuhatarisha usalama.
Alisema
kwa muda mrefu Jeshi lake limekuwa likimtafuta mtu huyo kutokana na
malalamiko mengi ambayo yamekuwa yakijitokeza na uchunguzi umebaini kuwa
jina lake haliko katika orodha ya watumishi wa Idara ya Usalama wa
Taifa.
Alisema
mtuhumiwa huyo alifanya tukio la mwisho ambalo limesababisha kukamatwa
kwake alipomtishia mfanyabiashara mwenye asili ya Kisomali, Abdul
Mohamed.
Alisema
alimtaka ampatiwe fedha kiasi cha sh. milioni 25 vinginevyo
angechukuliwa hatua chini ya Sheria ya Usalama wa Taifa. Alisema
mlalamikaji alitoa taarifa Polisi ndipo mtuhumiwa huyo alipokamatwa na
polisi. Alisema uchunguzi zaidi unaendelea.
Katika
hatua nyingine polisi wamefanikiwa kukamata bastola moja aina ya
Blowning namba zake zilifutwa ikiwa na risasi 11 ndani ya magazine.
Alisema
awali Polisi walibaini kundi la majambazi tisa waliokuwa wamevamia duka
kwa lengo la kupora mali ambapo walifanikiwa kumkamata mlinzi wa duka
hilo, Juma Adam (32) ambapo walijaribu kumfunga kwa kutumia kamba.
Wakati
huo huo, Jeshi la Polisi limeunda jopo la wapelelezi likiongozwa na
Mkuu wa Upelelezi Kanda ya Dar es Salaam, Costantine, kuchunguza na
kutoa taarifa sahihi kuhusu kifo cha Lebaratus Damiani, ambaye anadaiwa
kifo chake kimesababishwa na polisi.
Akizungumzia
kifo chake alisema kuwa, kabla ya mauti yake alikuwa amelazwa katika
Hospitali ya Muhimbili akiwa chini ya ulinzi wa askari wa Kituo cha
Stakishari.
Alisema
taarifa za awali zinaonesha kwamba marehemu alikuwa na ugomvi na
uhasama mkubwa kati yake na mtu aitwaye, Hamisi Magoma, ambapo katika
matukio mbalimbali walikuwa wakishambuliana kila walipokutana. Alisema
mara ya mwisho Damiani alikamatwa kwa kosa la kumjeruhi Magoma kwa
panga.

