Pingamizi la Mwanasheria Mkuu (AG) dhidi ya ombi la kibali cha kufungua kesi ya kupinga vikao vya Bunge Maalumu la Katiba vinavyoendelea mkoani Dodoma limetupiliwa mbali katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Pingamizi
hilo lilikuwa la kupinga ombi lililowasilishwa na Chama cha Wanasheria
wa Tanganyika (TLS) waliofungua kesi ya kikatiba wakiomba mahakama itoe
zuio la kuendelea kwa vikao vya Bunge maalumu la katiba hadi kesi hiyo
itakapokwisha.
Aidha,
wanaomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) awasilishe bungeni muswada
wa marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba namba 8 ya mwaka 2011
na namba 2 ya mwaka 2012, sura ya 83 na ifafanue kifungu cha 25 cha
sheria hiyo.
Uamuzi
huo ulitolewa jana na jopo la majaji watatu wanaosikiliza ombi hilo
wakiongozwa na Jaji Augustine Mwarija, Dk Fauz Twaib na Aloyisius
Mujulizi.
Wakati
huo huo, kesi nyingine ya kikatiba iliyofunguliwa na Mwandishi wa
Habari, Saidi Kubenea akihoji mamlaka ya Bunge hilo inaanza kusikilizwa
leo ambapo ilitakiwa ianze kusikilizwa jana lakini AG aliwasilisha
pingamizi ambalo pia litaendelea kusikilizwa leo.
Katika
kesi hiyo, Kubenea anaiomba mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya
Mamlaka ya Bunge la Katiba, kwa kuzingatia kifungu cha 25 (1) na (2) cha
Sheria ya Mbadiliko ya Katiba namba 83 ya mwaka 2011.
Aidha,
anaiomba mahakama itamke kama bunge hilo lina mamlaka ya kubadilisha
maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba na kwa kiwango gani.
