Na Francisca Emmanuel.
SHAHIDI wa kwanza katika kesi ya ubakaji
inayomkabili mume wa mwimbaji wa muziki wa injili, Flora Mbasha,
Emmanuel Mbasha (32) ameieleza mahakama jinsi alivyobakwa akiwa kwenye
gari na nyumbani kwao.
Shahidi huyo mwenye umri wa miaka 17 (jina
limehifadhiwa) ambaye pia ni shemeji wa Mbasha, alidai mbele ya Hakimu
Wilberforce Luhwago kuwa Mei 23 mwaka huu, Mbasha alimbaka kwa mara ya
kwanza wakati mkewe Flora akiwa hayupo.
Alidai siku hiyo, Flora na mumewe
walitoka kwenda kufuatilia CD za video zao za nyimbo huku mtoto wao
(jina tunalo) akiwa shuleni.
Alidai alishangaa kuona ghafla Mbasha
alirudi nyumbani peke yake na kumlazimisha kufanya mapenzi kisha
alimtukana na kumtishia kumdhuru endapo atatoa siri.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali,
Nassoro Katuga, shahidi huyo aliendelea kudai kwamba Mei 25 mwaka huu,
siku ya Jumapili walikwenda kanisani na waliporudi Mbasha alilalamika
kuwa ana njaa hivyo alimpa fedha kununua chipsi.
Alidai baada ya kula, Mbasha alimwambia waondoke nyumbani kwenda kumtafuta Flora ambaye hakuwepo nyumbani siku hiyo.
“Tulipanda gari aina ya Toyota Ipsum,
wakati tupo njiani aliniambia nikae kiti cha mbele pamoja naye kwani
nilikuwa nimekaa kiti cha nyuma. Nilikubali kukaa katika kiti hicho
ndipo aliniambia kuwa ananipenda hivyo tufanye mapenzi kwani
nimeshazoea,” alidai shahidi.
Aliendelea kuieleza mahakama kuwa baada
ya kukubali kukaa katika kiti cha mbele, Mbasha alipandisha vioo vya
gari na kulaza kiti alichokuwa amekalia mtoto huyo na kuanza kumvua
sketi yake na nguo za ndani.
Pamoja na hayo alimkaba shingo na kumziba mdomo kwa khanga ili asipige kelele na kumbaka kwa mara nyingine.
Shahidi huyo alieleza kwamba baada ya
kitendo hicho kuisha, Mbasha alishuka kwenye gari na kumuacha dada huyo
akiwa ndani ya gari na aliporudi alimtaka waendelee kufanya mapenzi
kitendo ambacho mtoto huyo alikataa.
Hata hivyo, alidai baadaye alimtafuta
Flora kwa simu na alipopokea hakumwambia kilichotokea hadi alipofika
Sinza kwa dada zake ambako walimweleza Flora kwa njia ya simu kitendo
alichofanyiwa na mumewe, huku akiwa haamini kilichotokea.
Alidai walitoka pamoja na dada zake
kwenda kuripoti katika kituo cha Polisi cha Sinza na polisi waliokuwepo
kituoni hapo waliwaamuru kutoa taarifa hizo katika kituo cha polisi
ambacho tukio la ubakaji limetokea.
Hivyo walirudi hadi kituo cha Polisi cha Tabata na kutoa taarifa.
Kwa mujibu wa sheria za Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, kifungu cha 186, kifungu kidogo cha tatu cha
sheria za mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 kinaeleza kuwa mashauri
yote ya ubakaji yanatakiwa kusikilizwa katika mahakama ya siri.
Wakili Katuga aliiomba mahakama hiyo
kusikiliza kesi hiyo katika mahakama ya siri kwa kuwa mtoto huyo yupo
chini ya miaka 18 na hairuhusiwi mtu yeyote asiyehusika kusikiliza
mashauri hayo. Kesi imeahirishwa hadi Septemba 12 mwaka huu.
Mbasha anashitakiwa kwa mashitaka mawili
ambayo Mei 23 mwaka huu, maeneo ya Tabata Kimanga Wilaya ya Ilala,
alimbaka mtoto wa miaka 17 nyumbani kwake. Pia alidaiwa Mei 25 mwaka
huu, alimbaka tena mtoto huyo ndani ya gari kinyume na sheria.