Mbunge wa Jimbo la Ubungo Jijini Dar es Salaam Mh. John Mnyika
anakusudia kumshtaki mahakamani Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda kwa kosa
la ofisi yake kushindwa kutangaza tarehe pamoja na maadalizi ya uchaguzi
wa serikali za mitaa.
Akizungumza
Jijini Dar es Salaam huku akiwa ameambatana na mwanasheria wake, Mh.
Mnyika amesema moja ya hoja zilizomo katika shauri watakalofungua kuwa
ni kutaka mahakama imlazimishe waziri mkuu Mh. Pinda, atoe kanuni pamoja
na kutangaza ni lini uchaguzi huo utafanyika baada ya kile alichodai
kuwa ni kuwepo kwa kimya kirefu kuhusu kufanyika kwa uchaguzi huo.
Mh. Mnyika amesema kuwa kwa mujibu wa sheria, Ofisi ya Waziri Mkuu
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inatakiwa itangaze pamoja na kutoa
kanuni za uchaguzi huo miezi miwili kabla ya mwezi Oktoba na kwamba
kitendo cha ofisi hiyo kukaa kimya hakileti tafsiri sahihi juu ya hatma
ya uchaguzi huo.
Mbali ya kutaka waziri mkuu atangaze kanuni na siku ya kufanyika kwa
uchaguzi wa serikali za mitaa, Mnyika amesema katika hoja zake ataiomba
mahakama iitake serikali ibadilishe taratibu na sheria zinazosimamia
uchaguzi huo ili uwe huru na wa haki.