Wakati Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro likimshikilia mkazi wa wilayani
Mvomero, Johnson Damian Mkude kwa msala wa kumchinja mdogo wake na
kupeleka kichwa kwa mganga wa kienyeji ili awe bilionea, jeshi hilo
linamshikilia mfanyabiashara mwingine maarufu mkoani hapa aitwaye Lyimo
kwa tuhuma za kumcharanga mapanga Damas Valeniani (36) ambaye ni
mlemavu wa ngozi (albino).
Jamaa huyo maarufu kwa jina la Mangi, anadaiwa kutenda unyama huo
wiki iliyopita usiku wa manane kwenye Msitu wa Milima ya Uluguru, Mtaa
wa Bingwa Kiwasi Juu, Kilakala, wakati mlemavu huyo, akiwa amelala.
Akizungumza na Ijumaa Wikienda, mlemavu huyo alisema:
“Nilikuwa nimelala, ghafla nikasikia mtu akiingia akiwa ameshika panga na kuanza kunikatakata huku akitaka kuninyofoa masikio yangu. Nilimtambua kuwa ni Lyimo ambaye ni jirani yetu.”
Alisema kuwa baada ya kuona hali hiyo, alijitetea vya kutosha na
kufanikiwa kuchomoka, kwa bahati nzuri mpwa wake, Mathias John alitokea
na kumsaidia huku wakipiga kelele za kuomba msaada lakini tayari alikuwa
amshamcharanga panga kichwani na kusababisha atokwe na damu nyingi.
Alisema kuwa kutokana na woga alioupata, aliogopa kulala hivyo alikimbilia kwa mjumbe wa mtaa wao, Filemon Gyuna ambako alipatiwa huduma ya kwanza.
“Polisi walifika nyumbani na kumkamata
mtuhumiwa na kumfikisha kwenye mkono wa sheria na mimi nikapewa PF-3 kwa
ajili ya matibabu kwenye Hospitali ya Mkoa wa Morogoro,” alisema Damas
kwa maumivu makali.
Akihojiwa na mwandishi wetu juu ya tukio hilo, mwenyekiti wa mtaa
huo, Ally Malekela alikiri kutokea kwa tukio hilo na kueleza kwamba
Lyimo alipewa saa 24 za kuhama kwenye mtaa huo.
Wananchi mbalimbali waliozungumza na Ijumaa Wikienda, walisema
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, SAC Leonard Paul, anatakiwa
kufanya kazi ya ziada ili kukabiliana na matukio kama hayo.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa Chama cha Maalbino Mkoa wa Morogoro, David Mganga alisema: “Natoa wito kwa jamii ielewe kuwa kiungo cha albino hakiwezi kumpa mtu utajiri au mafanikio, waache kututesa sisi maalbino.”
CHANZO:IJUMAA WIKIENDA