Jukwaa la Katiba Hapa nchini limeonya kuwa litahamisha maandamano ya
wananchi kutoka sehemu mbali mbali nchini, kwenda kufunga ofisi za
Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma.
Hatua hiyo itafikiwa iwapo mwenyekiti wake Mh. Samuel Sitta
hatasitisha vikao vya bunge hilo mara moja kutokana na kutokuwa na
umuhimu kwa nchi hasa baada ya kufikiwa kwa muafaka baina ya vyama vikuu
vya upinzania kwenye bunge la katiba.
Mwenyekiti wa Jukwaa hilo Bw. Deus Kibamba amesema hatua ya kutaka
kufunga ofisi za Bunge Maalumu la Katiba inatokana na kile alichoeleza
kuwa matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi zinazotumika kwa matumizi
yasiyo na tija.
Kwa mujibu wa Kibamba, kuendelea kwa bunge hilo hakuna mantiki yoyote
hivi sasa ambapo pia Jukwaa limependekeza Sitta pamoja na mwanasheria
Mkuu wa Serikali jaji Frederick Werema wasiruhusiwe kugombea nafasi
yoyote ya kisiasa kwa kipindi cha miaka kumi kutokana na kile ilichodai
kuwa ni kuhusika kwao katika kuvuruga mchakato wa katiba.
