Mshiriki kutoka Mtwara, Mwanaafa Mwinzago ameibuka kidedea katika Shindano la Tanzania Movie Talents (TMT) lililofanyika usiku wa kuamkia JUMAPILI kwenye Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Katika
shindano hilo ambalo washiriki 10 walikuwa wakizitolea macho Shilingi
milioni 50, Mwanaafa aliweza kuzoa kura nyingi zaidi na hivyo kujiwekea
kibindoni mamilioni hayo na kuwatimulia vumbi washiriki wengine.
Awali
kabla ya kutangazwa mshindi, Mwenyekiti wa Kampuni ya Proin Promotions,
Johnson Lukaza alitoa ahadi kwamba kampuni hiyo itajitolea kumsomesha
mtoto Mwanaafa ili aweze kufanikiwa kufikia malengo yake.
Mwanaafa
ndiye mshiriki mdogo kuliko wote katika shindano hilo lililoandaliwa na
Proin Promotions ambapo miongoni mwa majaji watatu, wawili walikuwa
waigizaji maarufu nchini, Single Mtambalike ‘Ritchie Rich’ na Yvonne
Cherie ‘Monalisa’. Jaji Mkuu alikuwa Roy Sarungi.
Mara
baada ya kutangazwa mshindi, Mwanaafa aliangua kilio cha furaha
kuonesha kutoamini kwamba amefanikiwa kunyakua mamilioni hayo huku
akihaha huku na kule kumtafuta mama yake jukwaani.
Hata
baada ya kuitwa na kukabidhiwa hundi ya Shilingi milioni 50 na
Mwenyekiti wa Proin Promotions, Mwanaafa aliendelea kububujikwa machozi
ya furaha kuonesha kabisa kutoamini kinachotokea usiku huo.

