Kutokana
na zao la Chikanda linalopatikana katika hifadhi ya taifa ya Kitulo
iliyopo Makete mkoani Njombe kuwa hatarini kutoweka, uongozi wa hifadhi
hiyo umejipanga kikamilifu kupambana na waharibifu wa zao hilo.
Kauli
hiyo imetolewa na Kaimu mkuu wa hifadhi hiyo Bw. Pius Mzimbe katika
mahojiano maalum na eddy blog iliyotembelea hifadhi hiyo kujua
walivyojipanga kupambana na ujangili dhidi ya zao hilo.
Bw.
Mzimbe amesema zao hilo lipo hatarini kutowena kutokana na watu wasio
waaminifu kuingia hifadhini humo bila kibali na kuanza kuchimba zao hilo
la Chikanda ambapo licha ya kusababisha uharibifu wa zao hilo lakini
pia wamekuwa wakiharibu mimea mingine pamoja na mazingira kwa ujumla.
Mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro (kushoto)akipata maelezo kuhusu zao la Chikanda.
"Lakini
tu nikuhakikishie ndugu mwandishi tumejipanga vizuri, wapo watu ambao
wamefungwa jela, wengine wamelipa faini na pia wapo ambao kesi zao zipo
mahakamani, na sisi tumejipanga kuimarisha doria na ulinzi wa kutoka
kuhakikisha watu hao hawaingii kwenye hifadhi na pindi wanapoingia basi
wanadhibitiwa mara moja" amesema Mzimbe.
Kwa
hivi sasa kutokana na uchunguzi walioufanya wamegundua soko la zao hilo
lipo nchi jirani hasa Zambia ambapo hutumia zao hilo kuandaa vyakula
maalum kwa ajili ya sherehe, na kutokana na zao hilo kuwepo katika
hifadhi ya Kitulo hulazimika kuuzwa kwa gharama kubwa.
Kwa
mujibu wa sheria za nchi ni kuwa zao la Chikanda ni nyara ya serikali
hivyo hairuhusiwi kuchimbwa hata kama zao hilo lipo nje ya hifadhi hivyo
kwa yeyote atakayekamatwa na zao hilo atachukuliwa hatua za kisheria
kwa kukamatwa na nyara za serikali kinyume cha sheria, hivyo hifadhi
hiyo kutoa wito kwa wananchi hasa wanaoizunguka hifadhi hiyo kutoa
ushirikiano kuhakikisha rasilimali zilizopo hifadhini humo zinaendelea
kuwepo na haziaribiwi na watu wasio waaminifu.
Na Eddy Blog, Makete