MKUU wa mkoa wa Singida, Dk Parseko Kone amemmwagia sifa tele diwani
wa kata ya Mwangeza, katika halmashauri ya Mkalama mkoani Singida, Petro
Mliga (CHADEMA) kwa kuwezesha kata yake kuibuka ya kwanza kukamilisha
ujenzi wa maabara.
Dk Kone alitoa kauli hiyo katika mji mdogo wa Iguguno wilayani
Mkalama wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara yake ya siku nne kukagua
maendeleo ya ujenzi wa maabara shule za sekondari katika halmashauri za
Mkalama na Iramba.
Alisema kuwa pamoja na diwani Mliga kuwa chama cha upinzani, ameweza
kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kiwango
cha hali ya juu na kwa muda muafaka.
Akionesha kufurahishwa na kazi nzuri aliyoifanya diwani huyo wa
CHADEMA, Dk Kone aliwataka madiwani wengine waende kata ya Mwangeza
kujifunza huku akisema kuwa mara alipokagua maabara hizo alilazimika
kumwomba diwani huyo arudi CCM.
“Nilimwambia kwa nini usirudi nyumbani lakini yeye akanijibu kwani
kuna shida gani kama natekeleza sera za CCM,” Dk Kone alikiambia kikao
hicho cha majumuisho.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa watu wa aina hiyo ndio viongozi
wanaotakiwa kwa kuwa mapambano yao huishia jukwaani tu lakini
wakishateremka jukwaani huchapa kazi kama kawaida.
“Hawa ni watu wanaogombea upinzani kwa nia ya kuwaletea wananchi wao
maendeleo. Huyu ambaye sera yao ni kupinga kuchangia anawapita nyie
wenye sera?” Dk Kone alihoji na kuwapa changamoto madiwani wa CCM .
