Mapendekezo ya Sheria ya Mgongano wa Maslahi miongoni mwa viongozi na watumishi wa umma, kutenganisha viongozi, mali na biashara zao, ili kuzuia ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma unaoendelea kutokea nchini yamewekwa hadharani.
Katika
mapendekezo hayo yaliyowasilishwa jana Dar es Salaam na mtoa mada
kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Gertrude Cyriacus,
pamoja na mambo mengine, viongozi wote wa umma na watumishi wa umma,
watatakiwa kuchagua kati ya mali na biashara zao na nafasi ya utumishi
wa umma.
Uchaguzi
huo utafanyika kwa namna mbili; moja kukabidhi biashara zote kwa
kampuni ya udhamini, ambayo itaendesha biashara hizo huku mtumishi
mwenye mali, akinyimwa taarifa muhimu za biashara yake.
Pili
mali na biashara ambazo kiongozi wa umma atakuwa nazo, ambazo zinaweza
kusababisha mgongano wa maslahi, atatakiwa kuziuza kabla ya kukubali
kazi ya kutumikia umma au kampuni ya udhamini, inaweza kuuza mali hizo
bila hata kumpa taarifa.
Kwa
mujibu wa mapendekezo hayo, kiongozi wa umma atatakiwa na sheria
kuweka mali zake katika kampuni hizo za udhamini, ambazo zitateuliwa na
kupewa masharti ya kuendesha biashara za viongozi.
Sheria
hiyo itatamka viongozi watakaohusika kuweka mali au biashara zao kwenye
kampuni hizo, ambao watakuwa viongozi wote wa kisiasa na viongozi
waandamizi.
Pia
mapendekezo ya sheria hiyo yameweka wazi aina za biashara ambazo
Kiongozi wa Umma, atatakiwa kukabidhi kwenye kampuni hizo, ambapo pia
kiongozi husika hatokuwa na madaraka yoyote kuhusu uendeshaji wa
biashara zake zitakazosimamiwa.
“Kampuni
za udhamini hazitatoa taarifa yoyote kwa kiongozi husika kuhusu
biashara zake, isipokuwa tu taarifa kuhusu thamani ya biashara husika,” alisema Gertrude wakati akiwasilisha mapendekezo hayo.
Aidha,
mapendekezo ya sheria hiyo yametamka muda wa mwaka mmoja kwa ajili ya
Kiongozi wa Umma kupata taarifa kuhusu kodi ya mapato na thamani ya
biashara alizoziweka katika kampuni za udhamini na taarifa hiyo itapitia
kwanza katika Sekretarieti ya Maadili.
Kwa
masharti hayo, kwa mujibu wa mapendekezo ya sheria hiyo, kampuni za
udhamini, zitatakiwa kuwasilisha taarifa za mali na shughuli za biashara
kila mwisho wa mwaka, kwa Kamishna wa Maadili kwa utaratibu
utakaowekwa.
“Kampuni
za udhamini zitakabidhi mali na biashara mara Kiongozi wa Umma
atapohitimisha muda wake wa uongozi. Aidha, kampuni ya udhamini
haitawajibika na hasara yoyote itakayotokea katika biashara husika, ili
mradi ifanye kazi yake kwa nia njema na kwa kufanya uamuzi wa busara,” imeelezwa katika mapendekezo hayo.
Ingawa
kampuni hizo za udhamini, zitakuwa na kinga, ikiwa biashara ya kiongozi
itapata hasara, pia kampuni hizo zimepewa mamlaka ya kuuza mali
ambazo zinaweza kumsababishia Kiongozi wa Umma kuingia katika
mgongano wa maslahi.
Mbali
na uwezo huo wa kuuza mali, viongozi pia wamewekewa zuio wasitoe
maagizo kwa kampuni ya udhamini, itakayoteuliwa kusimamia biashara
husika.
“Sheria
imtake kiongozi wa umma ambaye hataridhia kuweka mali zake kwenye
kampuni za udhamini, kuchagua kuuza mali ambazo zinaonekana zinaweza
kumuingiza kwenye mgongano wa maslahi,” imeelezwa.
Sheria
hiyo pia itazuia viongozi wa umma walioko madarakani, kujiongezea
maslahi ya aina yoyote na kama wakifanya hivyo, maboresho hayo ya
maslahi, hayatatekelezwa mpaka atakapoondoka katika cheo husika.
“Sheria
iweke masharti yatakayozuia kiongozi kushiriki kufanya uamuzi wa
uboreshaji wa maslahi, yanayohusu nafasi anayoitumikia na maboresho
yoyote yatakayofanyika, yaanze kutumika baada ya kiongozi husika
kuondoka katika wadhifa husika,” imeelezwa.
Lengo
la kipengele hicho, limetajwa kuwa ni kumfanya kiongozi atekeleze
majukumu kwa misingi ya haki, usawa na uaminifu kwa kuwa, Sekretarieti
ya Utumishi wa Umma, imebaini kuwa baadhi ya viongozi wenye dhamana ya
kusimamia taasisi za kuboresha maslahi, hutumia fursa hiyo kujinufaisha
binafsi kwa kuboresha maslahi kwa kipindi wanachokuwa madarakani.
Kuhusu zawadi, Sheria hiyo inatarajiwa kuzuia watumishi wa umma kutoa zawadi kwa wasimamizi wao wa kazi.
Lengo
la zuio hilo, ni kuondoa uwezekano wa kuathiri uamuzi kwa misingi ya
haki na usawa, kwa kuwa imebainika kuwa baadhi ya zawadi ni rushwa ya
kuwekeza, inayotolewa kwa malengo ya kujinufaisha baadaye.
Akizungumza
katika semina hiyo, mgeni rasmi, Rais wa Awamu ya Tatu, Ali Hassan
Mwinyi, alisema Serikali haijawahi kufuta Azimio la Arusha kama
inavyodaiwa na baadhi ya wananchi, bali ilizimua azimio hilo kuwapatia
viongozi wa kati, uwezo wa kumudu makali ya maisha.
Lengo
la kipato hicho kwa mujibu wa Mzee Mwinyi, ilikuwa kuwasaidia kumudu
mahitaji ya maisha na kupata haki ya kikatiba ya uhuru wa kuwa na mali
ya akiba ndogo, ili imuokoe mtumishi wakati wa dharura kama vile kuugua
au kufiwa.
“Ninyi
ni mashahidi kuwa hali hiyo ilikuwa kinyume cha matarajio, kwani watu
wamekuwa wakitumia vibaya haki ile ya kikatiba, kwa kumiliki mali hata
kwa njia zisizo halali… tuliwaruhusu kuingiza mkono, lakini wao
wakaingiza mwili mzima,” alisema.
Kamishna
wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Salome Kaganda,
alisema makusudi ya mapendekezo ya sheria hiyo ni kuleta amani na
utulivu wa nchi.
“Mapendekezo
ya sheria hii, hayalengi kuwafanya viongozi kuwa maskini, bali kasi yao
ya ukwasi iendane na hali halisi ya kipato chao.
“Lazima
kuwepo na hatua ya Serikali kurejesha maadili ya viongozi, kama
itazingatiwa na kuheshimiwa, Taifa litafikia maendeleo ya haraka
yaliyokusudiwa,” alisema Jaji Kaganda.
