Na Edwin Moshi, Makete.
Baadhi ya vyanzo vya maji vilivyoko katika kijiji cha Malembuli kata ya Mang'oto wilayani Makete mkoani Njombe vipo hatarini kukauka kutokana na watu kupanda miti siyo rafiki na mazingira katika vyanzo vya maji vilivyopo kijijini hapo.
Mwandishi wetu ambaye amefika kijijini hapo na kutembelea vyanzo viwili vya maji kwa nyakati tofauti ameshuhudia kuwepo kwa miti aina ya mipaini ambayo inakausha vyanzo vya maji ikiwa imepandwa karibu na vyanzo hivyo huku ikionekana kutunzwa vizuri ilihali haina faida yeyote katika vyanzo hivyo.
Imekuwa ikihamasishwa kutunzwa kwa vyanzo vya maji ikiwemo kupanda miti ambayo ni rafiki na mazingira ambapo katika vyanzo hivyo miti aina ya midobori ambayo ni rafiki wa mazingira imepandwa huku ikionekana miti mingine ambayo si rafiki ikizunguka vyanzo hivyo.
Mkazi mmoja wa kijiji hicho aliyeomba hifadhi ya jina lake ameitaka serikali ya kijiji kuchukua hatua kwa wahusika wote wanaoharibu vyanzo vya maji bila huruma ama woga kwa kuwa suala la kutunza vyanzo vya maji ni suala la kisheria.
"Hakuna haja ya mtendaji kuwaogopa wahusika, hapa sheria ichukuliwe kwani wenye miti wanafahamika, hakuna kucheka na mtu kwa kuwa vyanzo hivi vya maji vinahitajika sana na wanamakete wote" amesema.
Akizungumza na mwandishi wetu afisa mtendaji wa kijiji hicho Bw. Anton Ponela amekiri kuwepo kwa hali hiyo na kusema kuwa tayari wameshaanza kuchukua hatua kwa kuunda kamati ya watu wawili kila kitongoji kwa ajili ya kufuatilia uharibifu wowote unaofanywa katika vyanzo vya maji na kuwafikisha sehemu husika ili wachukuliwe hatua.
Amesema pia zimewekwa sheria ambazo zinatumika kuwabana waharibifu hao ikiwemo wanaofua nguo kwenye vyanzo hivyo, wanaopeleka mifugo yao, wanaokata miti kwenye vyanzo hivyo pamoja na wanaopanda miti isiyo rafiki na maji kwenye maeneo hayo.
Bw. Ponela ameongeza kuwa Agosti 22 mwaka huu wanatarajia kufanya kikao wao kama serikali ya kijiji ambapo pamoja na mambo mengine watajadiliana na kutoka na maamuzi kuhusu uharibifu wa vyanzo vya maji unaofanywa katika kijiji hicho ili wahusika wachukuliwe hatua.