
Mbunge wa Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ amelishutumu Jeshi
la Polisi mkoani humo kuwa ndiyo chanzo cha vurugu baada ya juzi
kutumia mabomu ya machozi kuwazuia wafuasi wa Chadema na waombolezaji
kuubeba mikononi mwili wa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Itiji,
Ezekiel King kwa lengo la kutembea nao kwa miguu kutoka Hospitali ya
Rufaa Mbeya hadi nyumbani kwake Itiji kuuzika.
Baada ya mabomu hayo kurushwa, viongozi na
waombolezaji walilazimika kulibwaga chini jeneza la mwili wa marehemu na
kuanza kukimbia.
Marehemu alifariki dunia katika hospitali hiyo,
alikopelekwa kwa ajili ya matibabu baada ya kuugua ghafla katika Gereza
la Ruanda alikokuwa akitumikia kifungo cha miaka saba baada ya
kupatikana na kosa la kudhuru mwili wa mwanachama wa CCM .
Akizungumzia tukio hilo, Sugu alisema kilichotokea juzi ni uthibitisho kwamba polisi ndiyo wamekuwa chanzo cha vurugu.
“Sisi tulikuwa kwenye msafara wakaja kutuzuia na
kuninyooshea bunduki. Tukawaeleza tunakwenda kuzika, wao wanasema
tulitakiwa kuomba kibali cha kwenda kuzika,” alisema Sugu na kuongeza:
“Watu walikuwa wengi na magari ya kuwabeba kwenda kuzika hayakuwepo, tuliamua kutembea sasa kibali cha nini,” alisema Sugu.
“Watu walikuwa wengi na magari ya kuwabeba kwenda kuzika hayakuwepo, tuliamua kutembea sasa kibali cha nini,” alisema Sugu.
Sugu alisema polisi wasipobadilika mara moja,
wananchi watachukua hatua kuwaondoa katika nyumba walizopanga uraiani
ili wakaishi kituo kikuu cha polisi mkoani humo kwa vile hawaijali jamii
inayowazunguka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi
aliwataka Chadema kuacha kuwazushia polisi na kuongeza kuwa madai ya
Sugu hayana ukweli wowote.