POLISI WANAOTUMIA PIKIPIKI WABANWA KISA RUSHWA

Sakata la nyendo zisizofaa zinazofanywa na baadhi ya polisi wanaotumia pikipiki (Tigo Fasta ) kumulikwa kikamilifu, limelizindua Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam na kuwaandikia barua watendaji wakuu wa kampuni ya The Guardian Limited  ili wakahojiwe sasa limechukua sura mpya ya kuiomba radhi kampuni hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa The Guardian Limited, Kiondo Mshana na Mhariri Mtendaji wa Nipashe, Jesse Kwayu,waliandikiwa barua ya kuitwa ili wakahojiwe na jeshi hilo kufuatia gazeti la NIPASHE kuandika habari iliyofichua vitendo vya askari hao kukamata magari ya mizigo na kudai rushwa.

Mshana na Kwayu waliwasili makao makuu ya Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam saa 4:00 asubuhi wakiwa wameambatana na Mwansheria wa Kampuni ya The Guardian na kuingia katika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa kanda hiyo na kuelezwa kuwa aliyewandikia barua ya kuitwa hajafika ofisini.

Saa moja baadaye aliwasili Mkuu wa Upelekezi Kanda Maalum Dar es Salaam, Jafari Ibrahim,baada ya kuona waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari  wakimsubiri alimuuliza katibu muhtasi wake kuna nini hadi wageni wamekuwa wengi katika ofisi yake na kujibiwa kuwa ni waandishi.

Kutokana na hali hiyo Mkuu wa Upelelezi Kanda ya Dar es Salaam, aliwaita waandishi wote ofisini kwake akiwamo Mkurugenzi Mtendaji The Guardian Limited na Mhariri Mtendaji Nipashe na kuanza kuzungumza nao.

Ibrahimu aliwaeleza kuwa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam hali mtu ambaye linamtuhumu na kwamba hata ofisi yake haijui ni nani aliyewaandikia barua ya kuitwa kuhojiwa Mkurugenzi Mkuu The Guardian Limited na Mhariri Mtendaji Nipashe.

Baadaye Mhariri Mtendaji Nipashe, Kwayu, alitoa barua walitoandikiwa ya kuitwa iliyoandikwa na kusainiwa na  Aman Makanyaga-SSP kwa niaba ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum Dar es Salaam na nakala kwa Kamishna wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam.

 Baada ya kuisoma barua hiyo yenye kumbu Na. DSMZ/CID/B.1/VOL.XX/128 ya Julai 21 mwaka huu,Mkuu wa Upelele Kanda Maalum Dar es Salaam, Ibrahimu alisema hana taarifa za barua hiyo na kwamba hata lugha iliyotumika katika barua hiyo haikuwa sahihi.

“Siyo kila kitu boss ajue lakini lugha aliyoitumia siyo sahihi alitakiwa aseme nawaomba tuonane au sisi ndio tuje ofisini kutaka ufafanuzi wa jambo fulani,nawaomba radhi kwa usumbufu mliopata,”alisema.

Mkuu huyo wa Upelelezi alisema aliwahidi kuwa atafuatilia suala hilo kubaini kilichojitokeza na kusisitiza kuwa ofisi yake haina taarifa yeyote ya kwamba kuna gazeti liliandika vibaya Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam.

“Vyombo vya habari ni moja ya ‘sorce’ nzuri ya Jeshi la Polisi, mnapoandika jambo lolote inatusaidia sisi kufuatilia jambo hilo na kulirekebisha haraka,nawaomba radhi sana kwa usumbufu mliopata tuendelee kushirikiana,”alisema.

Kufuatia kauli hiyo ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji The Guardian Limited, Mshana  alisema inashangaza askari huyo kuandika barua bila boss wake kujua.

“Mfano huyu (Mhariri Mtendaji) hawezi kuandika barua kwa niaba yangu bila mimi kujulishwa labla kama huyo mtu ana tatizo la elimu,”alisema. Mshana alisema atajitolea kuwafundisha polisi bure namna kazi zinavyofanyika kwenye media (vyombo vya habari) na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum Dar es Salaam akaomba awe wa kwanza kupewa elimu hiyo.

Aliongeza kuwa alisema askari huyo aliyeandika barua kwa kutambua kuwa amekosea wakati yeye (Mshana) akiwa hapo makao makuu ya polisi amempigia simu kumweleza kuwa amekosea kuandika barua hiyo.

“Mimi Managing Director ananiandikia barua tena kwa jina kuniita na mimi pia natuhumiwa kwa habari iliyoandikwa,”alisema.
 Kwa upande wake Mhariri Mtendaji Nipashe, Kwayu alisema kuna tatizo kwa Jeshi la Polisi kama inawezekana mtu anaandika barua bila kumjulisha bosi wake.

UTARATIBU MPYA WAWEKWA
Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum Dar es Salaam, Ibrahimu,alisema kutokana na malalamiko ya wananchi kuhusu askari wanaotumia pikipiki,wamelazimika kubadilisha utaratibu na sasa watakuwa chini ya Wakuu wa Polisi Wilaya (OCD) badala ya kuwa chini ya Kanda Maalum Dar es Salaam.

Alisema wamelazimika kufanya hivyo ili kuweza kuwathibiti askari polisi wenye vitendo vibaya.Gazeti la Nipashe Julai 18 mwaka huu lilichapisha haria ya uchunguzin kuhusu askari polisi wanaotumia pikipiki wanaofahamika kwa jina maarufu la Tigo Fasta, kwamba wamekuwa kero kubwa jijini Dar es Salaam, kutokana na kuacha kutekeleza jukumu lao la kupambana na uhalifu na kujiingiza katika vitendo vya kukamata magari ya mizigo na kudai rushwa.

Polisi hao wanalalamikiwa kwa kukamata malori ya mizigo zikiwamo Fuso na Pick Up, pamoja na kukamata magari mengine yanayokiuka sheria za usalama barabarani wakati ni jukumu la askari wa usalama barabarani.

Askari hao wanadaiwa kujiwekea utaratibu katika kila gari wanalolisimamisha kuwatishia madereva ili wawapatie kitu chochote.

MAENEO WANAYOPENDA
Maeneo ambayo NIPASHE ilipiga kambi na kufichua vitendo vya rushwa ni pamoja na barabara zinazoelekea Kariakoo hasa eneo la Jangwani kwenda Kigogo, Kamata, Morocco, Gongolamboto na barabara ya Shekilango.

Katika uchunguzi huo, polisi hao walionekana wakijadiliana na madereva wa magari na bodaboda kwa muda mrefu na kisha kuwaachia baada ya kuwezeshwa.
 
CHANZO: NIPASHE


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright 2025 EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo