Mwanamke Yasinta Rwechengura, mkazi wa Boko wilayani Kinondoni, Dar anayekabiliwa na kesi ya kutuhumiwa kumtesa hausigeli wake kwa miaka miwili (siku 730), amejikuta akihenyeshwa mahakamani.
Hayo yamemkuta juzi
alipofikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya
Kinondoni kujibu tuhuma zinazomkabili ambapo alikuwa akipokea amri
kutoka kwa askari na kumfanya kukosa raha.
Msala huo unagusa hisia za wengi ndiyo maana watu kutoka viunga
mbalimbali vya Jiji la Dar walifurika mahakamani hapo kusikiliza
mwenendo wa kesi hiyo iliyosomwa mbele ya Hakimu Mkazi, Boniphace
Lihamwike.
Akisoma kesi hiyo mahakamani hapo, wakili wa serikali ambaye alikuwa
upande wa jamhuri, Mohamed Salum alisema anaiomba mahakama hiyo
kutotoa dhamana kwa mtuhumiwa kwa sababu za kiusalama.
Sababu ya pili alisema bado hali ya mgonjwa ni mbaya na amelazwa kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kesi hiyo ambayo inafuatiliwa kwa ukaribu na wanaharakati wa haki za
binadamu, awali ilikuwa inasikilizwa na Hakimu Suleiman Mzava ambaye
juzi hakufika mahakamani hapo kutokana na uhamisho alioupata na badala
yake kesi hiyo ilitajwa kwa Hakimu Lihamwike.
Upande unaomtetea mtuhumiwa huyo uliokuwa ukiongozwa na wakili wa
kujitegemea, Msomi Gidion, uliiomba mahakama kumpa mteja wao dhamana
lakini ukagonga mwamba.
Hata hivyo, wakili Mohamed aliendelea
kuiomba mahakama kwa mara nyingine kutotoa dhamana kwa mtuhumiwa kwa
sababu alizozitoa awali.
Hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, alisema pande zote zilikuwa
na hoja akianza na upande wa mtuhumiwa ambapo alitoa ufafanuzi kuwa ni
haki yake ya kikatiba kupata dhamana lakini upande wa jamhuri nao
ulikuwa na hoja.
Hakimu huyo alisema kuwa shauri hilo kwa mara ya kwanza lilianzia
kwa hakimu mwingine na ndani ya faili la kesi hiyo hakukuwa na vielelezo
vyovyote hivyo kuirudisha kesi hiyo kwa hakimu kiongozi kwa ajili ya
kupangiwa hakimu atakayeisikiliza.
Baada ya hapo, mtuhumiwa alipandishwa kwenye karandinga na kurudishwa
mahabusu kwenye Gereza la Segerea, Dar kuendelea kuhenya hadi
atakapopata dhamana huku wananchi waliofika mahakamani hapo
wakimshangaa.