USHIRIKINA umetajwa kwa mahabusu wa Gereza la Wilaya ya Geita waliovua nguo mbele ya Mahakama ya Mwanzo ya Nyankumbu mkoani hapa wakimshinikiza Mkuu wa Mkoa wa Geita (Said Magalula), Jaji Mkuu (Mohammed Chande Othman) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (Stephen Werema) kusikiliza madai yao ya msingi.
Tukio hilo lilijiri Juni 26, mwaka huu saa 3:00 asubuhi ikiwa ni muda
mfupi baada ya kutoka mahakamani bila kesi zao kusikilizwa na kutakiwa
kupanda kwenye gari la polisi kurudishwa mahabusu.
Wakati sakata
hilo likiendelea, baadhi ya watu walisikika wakisema kuna uwezekano
madai ya mahabusu hao si waliyoyasema bali ni imani za kishirikina
kutoka kwa waganga.
“Unaweza kusema wanadai kusikilizwa, kumbe wanatumikia maelekezo ya
waganga, wengine wanaambiwa mkifika mahakamani vueni nguo, sasa
watavuaje watu wakawaelewa, si lazima wazue balaa la kutaka haki,”
alisema mkazi mmoja wa Geita.
Iliendeelea kudaiwa kuwa, wapo mahabusu wengi wanaofanya matendo ya
kuashiria ushirikina kwa sababu katika hali ya kawaida, si rahisi mtu
timamu kuvua nguo, wengi hutumia njia ya kugoma kula.
“Tunataka
haki, tumechoka kuonewa, watu tunasingiziwa kesi za mauaji, wengine tuna
kesi za wizi lakini kila siku kesi zinaahirishwa kwa madai eti hakuna
ushahidi, tumefika hapa leo tunaambiwa kesi zimeahirishwa,” walisikika
wakisema mahabusu hao.
Mahabusu hao pia waligoma kuingia kwenye gari la polisi na kubaki
wakiung’ang’ania mlingoti wa bendera ya taifa iliyo mbele ya mahakama
hiyo huku wakisema endapo wangepigwa wangeing’oa bendera hiyo.
“Vaeni nguo, mkuu wa mkoa hawezi kuja kuongea na watu mkiwa uchi hivi
halafu mpande kwenye gari twende gerezani tukazungumze,” alisema kaimu
ofisa usalama wa Mkoa wa Geita ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Mahabusu hao walikubali kuvaa nguo lakini wakaendelea na mgomo wa
kuingia kwenye gari, muda mfupi alifika Katibu Tawala wa Wilaya ya
Geita, Gasper Kanyaita kuzumgumza nao kwa niaba ya mkuu wa wilaya ndipo
wakakubali kuingia kwenye gari la polisi lenye namba za usajili PT 1166.