Na Rose Masaka-MAELEZO-Dar
es Salaam.
Serikali imewataka wananchi kujihadhari
na wizi ambao hufanywa na Taasisi za Fedha hewa ambazo zimekuwa zikidai kutoa
mikopo kwa njia ya simu.
Tahadhari hiyo
imetolewa leo na Mkurugenzi wa Idara ya Habari(MAELEZO) Assah Mwambene wakati
akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam.
Amesema kuwa Taasisi
hizo zimekuwa zikitumia mitandao ya simu
za mkononi kutapeli wananchi kwa kuwaraghai kuwa watawapatia mikopo.
Mwambene ameongeza kuwa
Taasisi hizo zimekuwa zikitumia majina ya viongozi wakubwa mbalimbali wa vyama
na Serikali kuwatapeli wananchi kwa kuwachukulia fedha zao.
Amesema kuwa baadhi ya taasisi
hizo zinatumia namba za uongo za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwaibia
wananchi.
Mkurugenzi huyo
amezitaja baadhi ya Taasisi hizo kuwa ni pamoja na Social credit Loans ambayo
inadai imesajiliwa na TRA kwa namba
Reg.No.33/SCC/REG/7894 na namba ya utambulisho wa mlipa kodi ni TIN:203-344-6789.
Taasisi nyingine ni
Saving Foundation na Quicken Loan ambazo zote hizo zimekuwa zinawatapeli
wananchi.
Amesema kuwa baada ya
kuwasiliana Mamlaka ya Mapato Tanzania, imebainika kuwa hakuna taarifa yoyote
kuhusu Taasisi hizo.
Mwambene amesema kuwa Serikali
inaendelea kufanyia uchunguzi ili wahusika waweze kukamatwa na kuchukuliwa
hatua.
Aidha, Mkurugenzi huyo amewakumbusha wananchi kutokubali maombi ya fedha, fadhila
au maelekezo yanayodaiwa kutolewa na uongozi wa juu bila kupata uthibitisho
kutoka mamlaka husika.