Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa amemtaka Waziri wa Afya
na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid kujiuzulu kutokana na sakata la
utupaji viungo vya binadamu katika Bonde la Mto Mpiji, Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla ya kuuaga uongozi wa
Chama cha Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wa Chadema (Chaso) na kufungua Tawi la
Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Tiba Muhimbili (Muhas) jana, Dk Slaa
alisema utupaji wa viungo hivyo ni udhalilishaji mkubwa wa binadamu na
kwamba Serikali inatakiwa kuwajibika moja kwa moja.
“Inashangaza kuona miguu, mikono, pua vinatupwa
dampo na Serikali na viongozi wake bado wamesimama. Halafu unafunga
hospitali ili umuathiri nani? Si unawaathiri wanafunzi wa chuo hicho
wanaoitumia kujifunza?” alisema na kuongeza:
“Nilitarajia waziri angejiuzulu tangu siku ya
kwanza baada ya kubainika vile viungo na asingejiuzulu basi Rais Jakaya
Kikwete amfukuze kazi.”
Dk Slaa alisema Serikali imelegalega katika
udhibiti wa viungo vya binadamu ambavyo hutumiwa na madaktari kujifunzia
kwa kukosa sheria madhubuti ya kudhibiti taratibu za matumizi yake.
“Niambieni kama kuna sheria ya kuharibu miili ya
binadamu hapa nchini na hivyo viungo vinavyoingizwa kutoka nchi za nje
vinaongozwa na sheria gani? Huwezi kuwa na madaktari halafu huna
sheria,” alisema Dk Slaa.
Mapema wiki iliyopita viliokotwa viungo vya
binadamu katika bonde hilo vikiwa katika mifuko myeusi na baadaye
vilibainika kuwa vilitoka katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na
Teknolojia (IMTU).
Tayari viongozi wanane wa chuo hicho wamekamatwa
na Polisi na Serikali imeunda timu ya wataalamu kuchunguza na mwishoni
wa wiki iliifungia Hospitali ya IMTU kwa kukosa sifa ya kutoa huduma za
matibabu.
Akisoma risala kwa niaba ya uongozi wa Chaso-Muhas
unaomaliza muda wake, mwenyekiti mstaafu wa tawi hilo, Elias Mwakapimba
alisema wanakabiliwa na changamoto za uhaba wa vifaa vya kusomea,
upendeleo wa ajira na kuzuiwa kufanya siasa chuoni.
Pia, wanafunzi hao waliiomba Serikali iongeze
bajeti katika sekta ya afya ili iliweze kuzalisha wataalamu wengi na
kuwapa motisha ya kufanya kazi kwa ufanisi.
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Mashariki na Pwani,
Profesa Abdallah Safari aliwataka wanafunzi hao kusimamia harakati za
mapinduzi ya kisiasa na kuwataka wasiogope vitisho vinavyotolewa na CCM.
“Kazi ya wasomi ni kujitoa muhanga ili kuwakomboa
wanyonge wengi… lazima msimame imara msiyumbishwe na mabwanyenye
wanaotaka kuyumbisha harakati zenu,” alisema Profesa Safari.