WATUMISHI 11 wa vitengo vinavyodhibiti
dawa za kulevya, wamekamatwa au kuhusishwa na biashara ya dawa za
kulevya katika maeneo mbalimbali nchini.
Hayo yamesemwa bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
wakati akijibu swali la Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile
(CCM).
Majaliwa alisema watumishi hao
waliokamatwa na kuhusishwa na dawa hizo, walikamatwa katika kipindi cha
mwaka 2012 hadi mwaka 2013.
Alisema watumishi hao walisimamishwa
kazi na kisha kushitakiwa mahakamani, ambapo baada ya kesi zao
kusikilizwa, wapo waliofungwa magerezani na kufukuzwa kazi.
Baadhi ya watumishi hao, kesi zao bado
zinaendelea mahakamani. Majaliwa alieleza kuwa mikakati inayochukuliwa
na Serikali ili kukomesha biashara ya dawa za kulevya ni pamoja na:
Kuundwa kwa Kikosi Kazi cha Kupambana na
Biashara ya Dawa za Kulevya mwaka 2006, Kuendelea kutoa elimu kwa umma,
hususan vijana kuhusu athari zitokanazo na dawa za kulevya na Kutoa
huduma ya tiba kwa watumiaji wa dawa za kulevya aina ya heroin, hasa kwa
wanaojidunga.
Mikakati mingine ni Kuongeza uangalizi
wa karibu katika maeneo ya mipaka, yanayotumiwa kuingiza dawa za
kulevya, kama vile viwanja vya ndege, bandari na mipaka ya nchi kavu;
Kutunga sheria mpya ya kupambana na
kuzuia biashara ya dawa za kulevya, itakayoanzisha chombo kipya chenye
mamlaka ya kukamata, kuchunguza na kupeleleza masuala yanayohusiana na
udhibiti wa dawa za kulevya nchini.
Majaliwa alisema pamoja na mikakati iliyopo na jitihada zinazofanyika, changamoto za kupambana na biashara hiyo ni nyingi.
Aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano
katika mapambano haya kwa kufichua wahalifu na kuwapeleka waathirika wa
dawa za kulevya katika vituo vya ushauri nasaha na matibabu, kupata
huduma.
Katika swali lake, Ndugulile alitaka
kujua watumishi wa vitengo vinavyodhibiti dawa za kulevya, wamekamatwa
au kuhusishwa na dawa za kulevya, hatua zilizochukuliwa dhidi yao na
mikakati ya Serikali kukomesha biashara hiyo.