SIKU moja baada ya mahabusu tisa wa gereza la Wilaya ya Geita mkoani
hapa kugoma na kuvua nguo hadharani mbele ya Mahakama ya Wilaya,
uongozi wa serikali jana ulilazimika kwenda gerezani kukutana nao.
Maofisa waliowatembelea mahabusu hao wametoka mahakama ya wilaya,
ofisi ya mwanasheria wa serikali pamoja na ofisi ya upelelezi wa makosa
ya jinai mkoa.
Akizungumza ofisini kwake jana, Hakimu
Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Geita, Desideric Kamugisha, alisema
walilazimika kuchukua hatua hiyo jana na wakafanya mazungumzo na
mahabusu pamoja na wafungwa kuhusiana na malalamiko yao ya kutotendewa
haki.
Alisema baadhi ya malalamiko hayo ni kuchelewesha kwa upelelezi wa
kesi zao hususani za mauaji na unyang’anyi wa kutumia silaha, huku
baadhi ya wafungwa wakidai kuhukumiwa adhabu kubwa tofauti na makosa
husika na kutokupata fursa ya kukata rufaa.
“Tumekubaliana nao na kuwataka waorodheshe malalamiko yote ambayo
wameyataja mbele yetu wakiainisha namba ya shauri, mwaka pamoja na
mahakama husika.
“Kazi hiyo imeanza tangu jana, kwa hiyo matokeo yataanza kujitokeza
muda si mrefu kuanzia leo, ili kumaliza kero hii,” alisema.
Kamugisha alisema kwa mujibu wa mwongozo wa kusikiliza kesi kwa
mwaka, mahakama inatakiwa kusikiliza mashauri 250, lakini wamejitahidi
kusikiliza kesi 436 tangu Januari hadi Mei mwaka huu, pamoja na kuwa na
upungufu wa hakimu mmoja wa wilaya na wawili wa mahakama ya mwanzo.
Mkuu wa Gereza la Geita, Joseph Mbilinyi, alisema wameanza kutekeleza
makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo hayo, ili kuondoa
malalamiko hayo.
Wakili wa Serikali Mkoa wa Geita, Mwasimba Hezeroni, alisema kuwa
changamoto walizopata walipotembelea gerezani humo watazifanyia kazi
kwa muda muafaka, na akataka kila upande utekeleze kazi zake kwa wakati
kwa maana ya mahakama, mwanasheria wa serikali pamoja na ofisi ya
upelelezi wa mkoa.
Mahabusu hao walichukua hatua hiyo juzi asubuhi muda mfupi baada ya
kutoka mahakamani bila kesi zao kusikilizwa na kulazimishwa kupanda
kwenye gari ya polisi kurudishwa mahabusu.
Na Valence Robert