Mkurugenzi
wa Takwimu za Kijamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Morice Oyuke
(kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini
Morogoro jana wakati akifungua Warsha ya siku moja ya kuwajengea uwezo
wanahabari kuhusu namna bora ya kuandika habari za kitakwimu. Kulia ni
Meneja wa Takwimu za Pato la Taifa, Daniel Masolwa.
Mtakwimu, Stephano Cosmas, akitoa mada katika warsha hiyo.
Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali wakiwa kwenye warsha hiyo.
Dotto Mwaibale, Morogoro
WAANDISHI wa Habari nchini wametakiwa kutumia taaluma yao kwa ajili ya kuhamasisha Umma kuhusu umuhimu wa Takwimu.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Takwimu za Kiuchumi Morice
Oyuke kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt.
Albina Chuwa mjini Morogoro jana wakati akifungua Warsha ya siku moja ya
kuwajengea uwezo wanahabari kuhusu namna bora ya kuandika habari za
kitakwimu.
"Ninyi wanahabari ni muhimu katika masuala ya takwimu hivyo ni
vizuri mjifunze jinsi takwimu zinavyoisaidia serikali, wadau wa
maendeleo na wadau wa takwimu katika kupanga Sera na kufanya tathmini ya
utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kama vile
Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 Tanzania Bara na mwaka 2020
Tanzania Zanzibar" alisema Oyuke.
Oyuke alitaja mambo mengine wanayopaswa kujifunza ni Mkakati wa
Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania Bara (Mkukuta) Mkakati wa
Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Zanzibar (Mkuza) na Mpango wa Taifa
wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2010/11 mpaka 2015/16 na Malengo ya Melenia
(MDGs)
Alisema eneo jingine watakalofundishwa ni kuhusu Pato la Taifa na
jinsi linavyokokotolewa na bei za ajira, takwimu za jamii na umuhimu
wake.
Dk. Chuwa alisema vyombo vya habari vinajukumu la kutoa taarifa
sahihi zilizo rasmi ambazo zinazalishwa na tafiti mbalimbali nchini ili
ziwafikie wadau wote nchini bila ya kupoteza maana.