WANANCHI WA TANDALA MAKETE WAIPONGEZA SERIKALI KUWAPATIA HUDUMA YA UMEME

Serikali kupitia shirika la umeme Tanesco wilayani Makete mkoa wa Njombe wamepongezwa kwa kuwasha umeme katika maeneo yaliyokuwa yakisubiri kupata umeme kwa muda mrefu sasa. 

Wakizungumza na mwandishi wetu baadhi ya wananchi wa kata ya Tandala wilayani Makete wamesema kutokana na umeme kuwaka katika baadhi ya maeneo kwenye kata hiyo kutasaidia kuharakisha shughuli za kimaendeleo zinazohitaji umeme. 

Bw. Emanuel Sanga ambaye amezungumza na ripota wetu amesema walikuwa wakisubiri umeme muda mrefu lakini kwa sasa wanaishukuru serikali kuwaletea umeme huku akiwaomba kuendeleza kasi ya kuendelea kuusambaza kwa kila mteja anayehitaji. 

"Kwa sasa ni baadhi ya nyumba za maeneo machache ndiyo zina umeme ila kwa sasa nawaomba tanesco waendelee kusambaza kwa kila mtu anayehitaji angalau na kata yetu sasa iwe na maendeleo" amesema Sanga. 

Amesema kwa sasa anatoa rai kwa wateja ambao hawajaomba kuunganishiwa umeme kwa kigezo kuwa hawakuwa na imani kuwa umeme utawaka katika kata hiyo, waombe ili nao waweze kuunganishiwa huduma hiyo muhimu. 

Mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Mbilinyi amesema umeme kuingia katika kata hiyo kutasaidia kuboreshwa kwa huduma zilizopo na hata kuanzisha huduma nyingine za kijamii ambazo zilikuwa zikihitajika lakini umeme ukakosekana akitolea mfano mashine nyingi za kusaga na kukoboa nafaka. 

"hapa wananchi wanategemea kusaga mahindi kwa mashine za mafuta ya dizeli na zipo chache sana, naimani kwa sasa kutakuwa na mashine nyingi za umeme na hata bei itapungua tofauti na kutumia mashine za mafuta" amesema Mbilinyi. 

Kwa hivi sasa Tanesco Makete inaendelea na zoezi la kuwaunganishia umeme wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo Ndulamo na Tandala


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo