CHAMA cha Walimu Nchini (CWT), kimeipongeza serikali kwa kukubaliana na hoja yao ya kuwa na mwajiri mmoja.
Akizungumza na waandishi wa habari, Rais wa chama hicho, Gratian
Mukoba, alisema CWT imefurahishwa na serikali kukubali kuunda chombo
kimoja cha kuwaajiri walimu nchini.
Alisema CWT ilianza kudai uwepo wa mwajiri mmoja kwa walimu tangu
serikali ya awamu ya tatu ili iwe rahisi kutatua kero za walimu nchini.
“Rais Benjamin Mkapa alisema angemwachia Rais wa awamu ya nne akisema
kuwa jambo hili linahitaji mabadiliko ya sera na sheria…Rais Jakaya
Kikwete alipoingia madarakani tunaamini alikabidhiwa jambo hili ambalo
tumekuwa tukilipigania kwa miaka kumi,” alisema Mukoba.
Mukoba alisema walimu nchini ni asilimia 64 ya watumishi wote wa umma
hivyo walihitaji chombo chao kimoja kitakachosimamia ajira yao kama
njia ya kumaliza migogoro ya mara kwa mara.
Alisema kwa kuwa azimio la Bunge limepitishwa , CWT inaishauri
serikali isijifungie ndani peke yake na kutoa chombo hicho bila
kuwashirikisha walimu.
“Tunachelea kisijekuwa chombo chenye majukumu yasiyokidhi na kusanifu
shida za ajira ya walimu ikiwemo usafiri, mishahara na kiinua mgongo,”
alisema Mukoba.
Aidha, alisema hatua ya kutawanya majukumu ya walimu katika mamlaka
mbalimbali kimesababisha kwa kipindi kirefu walimu kuishi na kero
zisizopatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Alisema kwa kuwa maandalizi ya katiba mpya yanafanyika CWT inashauri
chombo hicho kiwekwe kwenye Katiba mpya kama ilivyo kwa Kenya ambapo
chombo hicho kinafanya kazi vizuri.