MWENYEKITI wa Bunge, Mussa Zungu, amehoji kama ipo sababu ya mabasi ya abiria kukaa foleni ya mizani.
Zungu alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akiongoza kiti cha spika
baada ya swali la msingi la Mbunge wa Kilolo, Profesa Peter Msolla
(CCM).
Katika swali lake, Profesa Msolla alitaka kujua serikali ina mkakati
gani wa kurekebisha hali ya usumbufu wanaopata abiria kutokana na
msongamano mkubwa sehemu ya Kitonga.
“Kumekuwa na msongamano katika Wilaya ya Kilolo katika barabara ya
Dar es Salaam kwenda Zambia, hali inayosababishwa na ufunyu wa barabara
na mara nyingine kufungwa kabisa kutokana na ajali na kubomolewa
barabara kutokana na mafuriko,” alisema.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Gerson Lwenge,
alisema mabasi ya abiria kuwa na ulazima wa kupanga foleni inatokana
na sheria ya kuyataka magari yote yanayozidi tani tatu na nusu kupitia
kwenye mizani.
“Tutaiangalia sheria hiyo, ili tuone kama suala hilo linaweza kutafutiwa ufumbuzi na kubadilishwa,” alisema Lwenge.
Alieleza wizara inatambua umuhimu wa kuboresha usalama na kuondoa
usumbufu katika eneo la Mlima Kitonga lenye urefu wa kilomita 8
lililopo mkoani Iringa.
“Juhudi zilizofanywa na serikali ili kuboresha barabara katika eneo
la Mlima Kitonga, ni pamoja na ukarabati uliohusisha uimarishaji wa
barabara kwa kuweka tabaka la zege uliogharamiwa na Serikali ya Japan
kupitia JICA,” alisema.
Alisema barabara hiyo imekuwa ikifanyiwa matengenezo mbalimbali
yanayojumuisha uimarishaji wa maeneo ya kuegesha magari wakati wa
dharura.
Alifafanua kuwa pamoja na juhudi hizo, ili kupata suluhisho la kudumu
wizara imejumuisha mradi wa uimarishaji wa usalama katika Mlima
Kitonga kwenye mradi wa uimarishaji wa maeneo korofi yenye matukio mengi
ya ajali katika barabara ya TAZAM kuanzia Dar es Salaam hadi Tunduma
chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia.