Waziri
wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Sophia Simba akizungumza kabla
ya kufungua rasmi mkutano wa Kitaifa wa Kujadili Utokomezaji wa
Ukeketaji Nchini Tanzania.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Kitaifa wa Kujadili Utokomezaji wa
Ukeketaji Nchini unaofanyika Kunduchi Beach Hotel and Resort jijini Dar
es Salaam.
SERIKALI
imesema kitendo cha baadhi ya makabila kuendeleza mila za kuwakeketa
wanawake na watoto ni ukatili mkubwa ambao umekuwa na madhara kiafya kwa
anayetendewa. Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri
wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Sophia Simba alipokuwa akifungua
Mkutano wa Kitaifa wa Kujadili Utokomezaji wa Ukeketaji nchini Tanzania
unaofanyika kwa siku mbili katika Mkumbi wa Mikutano wa Kunduchi
Hoteli.
Waziri
Simba alisema ukeketaji ni udhalilishaji wa wanawake na watoto wa kike
na umekuwa ukihatarisha maisha ya wahusika kwa matokeo ya vifo, vilema
na maradhi kama vile fistula na magonjwa mengine hivyo kutaka kila mmoja
kuungana kuupinga.
Alisema kwa upande wa Serikali imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali
ili kuhakikisha inatokomeza mila hizo pamoja na ukatili mwingine wa
kijinsia.
“Wengi
hapa ni mashaidi wa madhara ya ukeketeji ikiwemo vifo, vilema na
maradhi kama vile, fistula na mengineyo. Serikali inalaani na kukemea
ukatili huu unaomdhalilisha mwanamke na kumletea madhara makubwa,”
alisema Waziri Simba.
Aidha alisema ili kupambana na hali Serikali imesaini mikataba
mbalimbali ya kukabiliana na ubaguzi anuai hasa kwa wanawake na pia
kuanzisha Dawati la Jinsia kila sekta kukabiliana na vitendo vya
kikatili nchini.
“…Serikali iliandaa na inatekeleza mpango wa taifa wa kuzuia na
kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (2001-2015) na mpango wa
kitaifa wa kutokomeza ukeketaji (2001-2015)…,” alisisitiza Waziri Simba.
Aliongeza
pamoja na hayo na juhudi mbalimbali za Serikali ukatili huo kwa
wanawake na watoto hauwezi kuzuiliwa kwa sheria na mipango ya serikali
hivyo kuitaka jamii pamoja na wadau wengine kuunganisha nguvu kupambana
na vitendo hivyo hapa nchini.
“….Suala la kutokomeza ukatili wa kijinsia, halitakwisha kwa kutegemea
Serikali au sheria peke yake. Ni jukumu letu wadau wote kwa pamoja
kukemea na kupiga vita kwa nguvu zote, kutoa elimu dhidi ya ukatili,
huduma kwa wahanga na kuhakikisha wanaotenda na kubariki vitendo hivi
wanachukuliwa hatua,” alisema.
Akizungumza
katika mkutano huo, Naibu Mwakilishi wa UNFPA Tanzania, Mariam Khan
alisema licha ya juhudi zinazofanywa kupambana na ukeketaji nchini, kila
mwaka vipindi vya ukeketaji bado wasichana na watoto wanaokeketwa
wamekuwa wakipoteza maisha bila sababu ya msingi kutokana na madhara ya
ukeketaji jambo ambalo haliwezi kuvumiliwa.
Aliwataka washiriki kwa pamoja kujadiliana nini cha kufanya ili
kukomesha ukatili huo unaoendelea kushamiri nchini na kuahidi kuwa UNFPA
itaendelea kuunga mkono juhudi za mapambano hayo kwa kutoa mafunzo na
kuwezesha shughuli za mapambano hayo.
Awali
akizungumza, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake
Tanzania (TAMWA), Valerie Nsoka alisema mkutano huo umewashirikisha
wakuu wa mikoa, viongozi wa dini, wawakilishi wa madawati ya jinsia na
wadau wengine kutoka mikoa yenye vitendo vya ukeketaji pamoja na asasi
zinazopambana na ukeketaji.
Aliongeza kuwa mkutano huo utafanyika kwa siku mbili ambapo wajumbe,
watapeana uzoefu na kufanya majadiliano ya kina kabla ya kuibuka na
mpango kazi wa nini kifanyike kutokomeza vitendo vya ukeketaji nchini.
Mkutano huo ulioratibiwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania
(TAMWA) umefadhiliwa na Shirika la UNFPA, Tanzania.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com