MWIZI ALIYEOKOLEWA KIFO NA POLISI WILAYANI MAKETE, ATUPWA JELA BAADA YA KUKIRI KOSA

Mahakama ya mwanzo  Makete  imemhukumu Bw.Hekima Mbilinyi (27) mkazi wa Ipelele kwenda jela mwaka mmoja na kulipa fidia ya 500,000/= kwa mlalamikaji Meneja Mbilinyi mkazi wa Maleutsi kata ya Iwawa wilayani Makete baada ya kuiba viatu jora moja na fedha taslimu sh. 350,000/=

Akitoa hukumu hiyo Hakimu wa Mahakama hiyo ya Mwanzo Mh.Happy Ngogo amesema hukumu hiyo imetolewa baada ya kujiridhisha na ushahidi ulitolewa mahakamani hapo ambapo   mtuhumiwa  huyo  alitenda kosa hilo Mei 27 mwaka huu, katika kijiji cha Maleutsi ambapo alibomoa nyumba ya mlalamikaji na kuiba jora moja la viatu lenye thamani ya shillingi 480,000/=

Akiwa mahakamani hapo mshitakiwa huyo amekiri kutenda kosa hilo na baada ya kupewa nafasi ya kujitetea ameiambia mahakama hiyo kuwa ana watoto wa tatu wanaomtegemea hivyo ameiomba mahakama hiyo kumpunguzia adhabu lakini hakimu ameamuru kuwa atatumikia kifungo cha mwaka mmoja jela na fidia ya shilingi 500,000/= kwa mlalamikaji  ambayo itatolewa baada ya kifungo hicho kumalizika

TUJIKUMBUSHE ILIVYOKUWA
Awali mtuhumiwa huyo alinusurika kuuawa na wananchi walioamua kujichukulia sheria mkononi katika kijiji  cha Maleutsi hivyo polisi kuamua kutumia nguvu za ziada (mabomu ya machozi) kumnusuru asiuawe na wananchi 

Katika hali isiyokuwa ya kawaida wananchi hao waliendelea kuwa wakaidi kwa amri za polisi ambapo mwandishi wa edwinmoshi.com aliyekuwepo katika eneo la tukio alinusurika kupokonywa vitendea kazi vyake kwa kile wananchi hao walichokiita kuwa hawataki vyombo vya habari  eneo hilo 

Aidha katika tukio hilo hakuna aliyepoteza maisha na jeshi la polisi wilayani hapa limetoa rai kuwa wananchi wawe na subira pindi wanapo mkamata mtuhumiwa wa uhalifu wowote kwani kujichukulia sheria mikononi ni kosa la jinai

Na Riziki Manfred wa Eddy Blog Makete


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo