Kifo
cha Mkazi wa kitongoji cha Ikandilo kata ya Mwendakulima wilayani
Kahama Mkoani Shinyanga Butamo Maziku (80) aliyedaiwa kuuawa na Fisi
usiku wa kuamkia jana, kimechukua sura mpya baada ya kubainika ni
uongozi umedanganya umma.
Siri
hiyo imefichuka jana baada ya Jeshi la Polisi wilayani humo kufika
kwenye tukio na kuthibitishiwa kwamba Marehemu Maziku aliuawa na watu
akiwa nyumbani kwake na kutupwa kwenye vichaka ili ijulikane kuwa
ameuawa na Fisi.
Juma
Kabado mjukuu wa Marehemu Butamo aliyehojiwa na kuachiwa huru
amekaririwa akiuambia umma kwamba, katibu wa Sungusungu wa sehemu hiyo
Athumani Kisaka aliwaelekeza watu waseme Butamo ameuawa na Fisi
vinginevyo wangeweza kusumbuliwa.
Imeelezwa, baada ya maelekezo hayo, Kisaka pia aliwaambia ndugu na
majirani waseme marehemu Maziku alikuwa akiishi bila ndugu kijijini hapo
wakati anao wajukuu wawili; Juma Kabado na dada yake aliyetambulika kwa
jina la Regina aliyedaiwa kutoroka.
Jamii imegubikwa na mashaka kufuatia madai kwamba Marehemu Butamo
aliuaawa usiku wa kuamkia jana, wakati damu iliyokutwa nyumbani kwake
imeonesha kuwa ina siku nyingi, na mwili wake umekutwa umeharibika
vibaya vichakani humo.
Watu saba wameshikiliwa na Jeshi la polisi kufuatia upotoshaji wa
taarifa hizo akiwemo Fredrick John (Mme wa Rebeka ambaye ni Mjukuu wa
Butamo), na Athumani Kisaka (Katibu wa Sungusungu), anayedaiwa
kusingizia Butamo kuuawa na Fisi.
Wengine wanaoshikiliwa na Jeshi hilo ni, Shaaban Juma, Jummanne Ally,
Hamis Rashid, Mayala Maganga na Luhumbika Lubigili, wote wakazi wa
kijiji hicho na ndiyo walioshiriki katika kutoa taarifa za uongo kwa
Jeshi la Polisi.
Na Marco Mipawa-Kahama