WAJUMBE wa Baraza Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
Mkoa wa Pwani, wamelikana kundi la watu waliojitokeza hivi karibuni
wakijiita viongozi wa chama hicho na kufanya mikutano yenye lengo la
kukichafua na kuwataka viongozi wa kitaifa wajiuzulu.
Kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Pwani, Said
Ukwezi, alisema kuwa wamelazimika kutoa tamko hilo baada ya kubaini
kwamba wanaofanya mikutano hiyo na vyombo vya habari si wanachama wa
chama hicho.
Ukwezi alisema kuwa hivi karibuni kumezuka mtindo wa kukichafua chama
hicho, ambao unaratibiwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa
mgongo wa waliokua viongozi wa CHADEMA wakafukuzwa na kutimkia
ACT-Tanzania.
Alisema kuwa kundi hilo limewahadaa Watanzania kwa kujitambulisha kuwa
ni viongozi wa CHADEMA, huku wakiwa mstari wa mbele kushiriki bila
kificho kazi na majukumu ya ACT-Tanzania, kama kugawa kadi na
kushawishi watu kuhama CHADEMA.
“Mtakumbuka Juni 23 mwaka huu, kundi hilo liliitisha mkutano na
waandishi wa habari katika Hoteli ya Lamada jijini Dar es Salaam na kwa
kiasi kikubwa mkutano huo uliitishwa kwa lengo la kuchafua hali ya
hewa na kujaribu kuwaaminisha Watanzania kuwa hali ya CHADEMA ni tete,
lakini ukweli wa mambo ni kuwa hali ya chama chetu ni shwari,” alisema.
Kwa mujibu wa Ukwezi, wanakosa majibu sahihi kuhusu ajenda ya kundi
hilo kwani katika kipindi hiki chama hicho kipo katika uchaguzi ngazi
ya kata na Septemba watakamilisha ngazi ya taifa, hivyo kama kundi hilo
limeona viongozi hao hawafai lingesubiri wakati wa uchaguzi mkuu
badala ya kukimbilia kutoa matamko yasiyo na tija.
Katika tamko lao, wajumbe hao wameeleza kuridhishwa na viongozi wa
kitaifa waliopo madarakani kutokana na kuongeza idadi ya wanachama
kuanzia ngazi ya vitongoji, mitaa, kata, wilaya hadi mikoa.
Kwamba kupitia viongozi hao wa kitaifa, programu ya CHADEMA ya msingi
imefanikiwa kukipeleka chama kuwa mtandao mkubwa na kuweza kukabiliana
na hila za CCM.