BALOZI wa zamani wa Vatican katika Jamhuri ya Dominica, Monsinyori
Jozef Wesolowski ametiwa hatiani na Mahakama ya Kanisa Katoliki kwa
tuhuma za kudhalilisha watoto.
Kutokana na kutiwa hatiani huko amepokwa upadre wake. Monsinyori
Wesolowski amekuwa kiongozi wa juu kuteuliwa na Papa kutiwa hatiani na
kupewa adhabu hiyo ya kupokwa upadri.
Taarifa ya Vatican ilisema Monsinyori Wesolowski alikutwa na hatia na
Mahakama hiyo ya Usharika wa Mafundisho ya Imani katika siku za hivi
karibuni: kwa adhabu hiyo ina maana hataweza kutekeleza majukumu yake
kama Padre.
Wesolowski amepewa miezi miwili ya kukata rufaa. Lakini pia
anakabiliwa na mashtaka katika Mahakama ya Makosa ya Jinai ya Vatican.
Kwa kuwa ni Mwanadiplomasia wa Kipapa yeye ni raia wa mji wa nchi hiyo.
Papa alimrejesha Vatican, Wesolowski ambaye ni mzaliwa wa Poland
Agosti 21, 2013 na kumfuta kazi baada ya Askofu wa Santo Domingo,
Kadinali Nicolas de Jesus Lopez kumueleza Papa Francis kuhusu kuwepo kwa
tetesi kuwa Wesolowski aliwadhalilisha watoto wa kiume akiwa Jamhuri ya
Dominica.
Mamlaka za Dominican hatimaye zilianza uchunguzi lakini hazikumshtaki. Poland, pia ilianza uchunguzi dhidi ya Wesolowski.
Wesolowski ni Ofisa wa Juu Vatican kuchunguzwa kwa tuhuma za
udhalilishaji watoto na kesi yake iliibua waswali iwapo Vatican, kwa
kumuondoka katika mamlaka ya Dominica ilikuwa ni kumlinda na kuanzisha
uchunguzi wake kabla ya mamlaka za taifa hilo la Caribbean.
Hata hivyo Vatican haijawahi kusema iwapo Wesolowski alishawahi
kujitetea kuhusiana na tuhuma hizo na hajawahi kutoa mawasiliano yoyote
kwa mawakili wake.
Kesi hiyo imekuwa ikichukuliwa kwa umakini kwani Wesolowski alipewa
upadirisho wake na Uaskofu na Papa St John Paul 11 ambaye pia ni Raia wa
Poland.