Mtu mmoja
Jabiri Joseph anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 25 hadi 30 amekufa
baada ya kujinyonga kwa kutumia mkanda wa suruali yake.
Kwa mujibu wa
polisi, mtu huyo inasadikiwa alijitundika kwenye nondo ya dirisha la chumba cha
nyumba alimokuwa akiishi.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kinondoni, jijini Dar es Salaam Camilius Wambura alisema hayo
jana na kuongeza kuwa tukio hilo limetokea juzi jioni katika Kata ya Mabibo.
Kamanda
Wambura alisema polisi walikuta mwili wa marehemu ukiwa umeketi kitandani kwake. Hata hivyo alisema kwamba chanzo cha
kifo kinaendelea kuchunguzwa na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali
ya Taifa Muhimbili.
Katika hatua
nyingine, polisi waliendesha msako katika maeneo ya Mburahati, Manseze, Mabibo
na Kigogo na kuwakamata watuhumiwa 50 wakiwa na kete 155 za bangi, misokoto 50
na pombe haramu ya gongo lita 75.
Watuhumiwa hao
ni Juma Shinda (36), Tabaya Alex (37), Abdi Juma (25), Sudi Idd(33), Rosemary
Mohammed(30), Mariamu Bakari (50) na wenzao 44.
Aidha katika
tukio jingine, Kamanda wa Polisi mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alisema watu 10 wamekamatwa kwa tuhuma za
kukutwa na bangi puri sita pamoja na pombe haramu ya gongo lita nane.
Watuhumiwa hao
ni Laurent Vicent (40), Lisa Johannes(33), Ali Said(32) na wenzao saba.
Watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.