WAFANYAKAZI WILAYANI MAKETE WASHAURIWA KUTUMIA VYAMA VYAO IPASAVYO KUTATUA KERO

 Katibu tawala wilaya ya Makete Joseph Chota, akihutubia wafanyakazi.

Wafanyakazi wilayani Makete mkoani Njombe wametakiwa kuvitumia vizuri vyama vyao vya wafanyakazi kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili

Kauli hiyo imetolewa leo na katibu tawala wilaya ya Makete Bw. Joseph Chota ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani (Mei Day) kwa niaba ya mkuu wa wilaya yaliyofanyika kiwilaya katika viwanja vya mabehewani Makete mjini

Amesema mbali na kuvitumia ipasavyo vyama hivyo pia wafanyakazi wanatakiwa kuendelea kufanya kazi kwa mshikamano na umoja wa hali ya juu ili kufanikisha malengo yaliyowekwa na vituo vyao vya kazi

Bw. Chota amesema pamoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi, serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kadri ya fedha zinavyopatikana na kuwaomba wafanyakazi kutokata tamaa ama kupunguza ari ya kufanya kazi kwa bidii

Awali Bw. Isaac Kilongo akisoma risala ya wafanyakazi mbele ya mgeni rasmi amesema wanaiomba serikali kuacha kuwakata mshahara wa wafanyakazi bila makubaliano nao huku akitolea mfano mchango wa mwenge ambao umekuwa ukikatwa mara moja kwa mwaka bila idhini yao

Amesema pia wanaiomba serikali kuwalipa posho wafanyakazi wanafanya kazi kwenye wilaya ngumu kimazingira ikiwemo Makete kwa tayari ilishapitishwa na serikali kuwa wafanyakazi hao watalipwa posho, pamoja na kuboreshewa mishahara yao kulingana na hali ya maisha ilivyo kwa sasa

Katika maadhimisho hayo wafanyakazi bora kutoka katika idara mbalimbali za halmashauri ya wilaya ya Makete wamepewa zawadi zikiwemo vyeti na fedha taslimu, michezo mbalimbali kama uvutaji kamba, kukimbia kwa magunia, kushindana kunywa soda pamoja na mpira wa volebo

Pia mgeni rasmi alipata wasaa wa kutembelea mabanda ya idara za halmashauri yaliyokuwepo uwanjani hapo na kupatiwa maelezo ya namna idara hizo za serikali zinavyofanya kazi

Kauli mbiu ya mwaka huu ni "utawala bora utumike kutatua kero za wafanyakazi"


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo