Askofu mkuu wa kanisa la PEFA Moivaro, lililopo Wilayani Arumeru, mkoani Arusha, Charles Nkya, juzi amenusurika kupigwa na waumini wake kanisani baada ya kuibuka vurugu kubwa ya kugombea madaraka....
Vurugu
hizo zilitulizwa na askari wa kutuliza vurugu FFU, waliokuwa
na silaha za moto pamoja na mabomu ya machozi ambao
walimuokoa askofu huyo...
Hali
hiyo ilitokana na baadhi ya waumini kukerwa na kitendo cha
Askofu Nkya kuwabadilishia mchungaji wasiyemtaka na kutangaza
kuwatenga baadhi ya waumini kwa madai ya kunuka dhambi...
Tukio
hilo lilichukua zaidi ya saa sita hadi kutulizwa kwake ambapo
waumini waligoma kuingia kanisani baada ya kupata taarifa kuwa
askofu wao alitaka kubadilisha uongozi wa kanisa hilo na
kumwondoa mchungaji wao, mama Nai Solomoni
Kabla
ya muda wa ibada kufika,waumini waliofika kanisani hapo mapema
walipigwa na butwaa baada ya kukuta kanisa hilo limevunjwa
mlango wa kuingilia hivyo kuzua hofu ya kutegwa mabomu...
Waumini
hao walilazimika kuita polisi toka kituo cha polisi Usa
River ambao walifika kanisani hapo kufanya upekuzi na kubaini
hakukuwa na dalili zozote za kutegwa bomu, hivyo baadhi yao
waliingia kanisani.....
Hata
hivyo, waumini wengine waligoma kuingia kanisani wakishinikiza
askofu Nkya kutofanya uteuzi wowote wa mchungaji lakini askofu
huyo alishinikiza na kutangaza kumteua mchungaji , Hyness Munuo
ambaye ni mke wa mwanzilishi wa kanisa hilo, marehemu mchungaji
Elibariki Munuo.....
Mbali
na uteuzi huo, askofu Nkya alitangaza kuwafukuza baadhi ya
waumni aliodai wanamuunga mkono mchungaji Solomoni ambapo hatua
hiyo iliibua vurugu kubwa kwa baadhi ya waumini ambao walimjia
juu askofu wao na kuanza kumshambulia kwa matusi, wengine
wakimtupia viti vya kukalia wakitaka warudishiwe fedha
walizochangia ujenzi wa kanisa hilo.....
Kutokana
na vurugu hizo, polisi walipata taarifa, wakafika eneo la tukio
na kuwaweka chini ya ulinzi baadhi ya waumini na kumtaka
askofu huyo na wasaidizi wake kuripoti kesho katika kituo cha
polisi cha Usa River ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa....
Mkuu
wa upelelezi wilayani humo, OC CID Jumanne Mkwawa, alimtaka
askofu Nkya kusitisha mabadiliko ya uongozi wa kanisa hilo
kama alivyotangaza hadi hapo mwafaka utakapopatikana
