Wabunge nchini Uganda wamepitisha mswaada unaotoa adhabu kali kwa watu wanaowaambukiza wengine virusi vya HIV kwa maksudi.
Mswada huo unapendekeza adhabu ya kifungo cha
hadi miaka 10 kwa wale wanaopatikana na hatia na pia inapendekeza
wanawake wajawazito na wapenzi wao kupimwa virusi vya HIV.
Mbunge mmoja kwa jina Peter Aleper
aliambia vyombo vya habari kuwa watu wanaowaambukiza wenzao virusi vya
HIV kwa maksudi ni hatari kwa jamii.
"ni lazima waadhibiwe vikali kwa sababu
kumuambukiza mtu HIV wakati unafahamu vyema kuwa wewe ni mwathiriwa ni
uuhalifu,'' alisema mbunge huyo. Ni hatari sana kwa sababu mru huyo
anaweza kuichanganya jamii na kumaliza watu.''
Lakini wafanyakazi katika sekta ya afya pamoja
na mashirika ya kutetea haki za wanyonge, wamepinga vikali mswada huo,
wakisema kwamba haitafanya lolote kudhibiti ongezeko la visa vya
maambukizi.
Wengi wanasema kuwa mswada huo utaongeza tu
unyanyapaa kwa watu wanaoishi na virusi hivyo. Pia wanasema kuwa watu
watahofia kupimwa kwa hofu ya kutengwa na jamii.
Mswada wenyewe umepitishwa baada ya sheria kali
inayopinga vitendo vya mapenzi ya jinsia moja kupitishwa na rais Yoweri
Museveni mwezi Februari.
bbc
