Siku chache baada ya kifo cha mwongozaji na mwigizaji wa filamu Bongo, Adam Philip Kuambiana, daktari mkubwa wa mastaa ameibuka na kudai marehemu alijiua mwenyewe.
Kwa mujibu wa daktari huyo ambaye hakupenda jina lake liandikwe kutokana na maadili ya taaluma yao kuficha siri ya mgonjwa,
siku moja kabla ya kifo (Ijumaa ya Mei 16, mwaka huu), marehemu
alimpigia simu na kumwambia amekunywa dawa za malaria aina ya Fansidar
lakini pia amekunywa pombe.
Daktari huyo alieleza kuwa, marehemu
alimpigia simu kumuomba ushauri juu ya nini cha kufanya na kama kuna
madhara yoyote juu ya pombe hizo na dawa alizokunywa.
“Aliniuliza kama kuna madhara yoyote ambayo anaweza kuyapata kwa kuwa
alikuwa amekunywa fansidar kwa ajili ya malaria kisha akapata kiu ya
bia na kuamua kunywa,” alisema daktari huyo.
AMSHAURI KWENDA HOSPITALI
Akizidi kuzungumzia
tukio hilo, daktari alikwenda mbele kwa kusema licha ya msanii huyo kuwa
na ‘masikhala’ mara kwa mara, lakini kwa kuwa alimwambia jambo ambalo
linahusu uhai wake, alimshauri kwenda hospitali iliyo karibu ili
akaonane na daktari kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kutoa sumu kwani
kitaalam mtu anapokunywa pombe akiwa amemeza dawa za aina hiyo vyote
hugeuka kuwa sumu.
Alisema kutokana na jinsi alivyozidi kumsimulia hali aliyonayo,
aliamini kwamba marehemu alikuwa anamaanisha alichokuwa akikisema hivyo
ikabidi amsisitize kuwahi hospitali haraka.
“Nilimwambia awahi hospitalini haraka kwani nilijua fansidar ni kali
na si dawa ya kufanyia mchezo. Lakini kesho yake nilipopata taarifa za
kifo chake niliumia sana japokuwa nilijua amejiua kwa kuchangaya
fansidar na bia maana mchanganyiko wa sumu yake mwilini ni mkali sana,”
alisema daktari huyo huku akisisitiza kusitiriwa kwa jina lake.
MAZINGIRA YA KIFO
Kwa mujibu wa mtu ambaye
alikuwa karibu na Kuambiana siku ya tukio ambaye naye hakutaka kutajwa
jina, marehemu asingekufa ghafla kama tatizo alilokuwa nalo
lingekuwa la vidonda vya tumbo ambavyo vilikuwa vikimsumbua kwa muda
mrefu.
“Siku ile marehemu alikuwa na pesa, alikunywa sana pombe kutoka
asubuhi mpaka usiku mwingi, alikuwa anakula kila anapojisikia sasa
hatuelewi ni kitu gani kilitokea maana haiwezekani mtu akutwe anaendesha
na kutapika damu pasipo kuwa na sumu mwilini,” alisema mtu huyo.
DAKTARI AWAASA MASTAA
Katika hatua nyingine,
daktari huyo aliwashauri mastaa wengine kuwa makini kwani mara kadhaa
amepata kesi za namna hiyo ambapo wanakunywa pombe vilabuni usiku huku
wakiwa katika dozi ya ugonjwa fulani.
“Mimi nawaambia ndugu zangu, hasa mastaa waache tabia ya kunywa pombe
wakiwa katika dozi, starehe zipo tu. Ni vyema wakawa wanauliza kwa
wataalam wa afya pindi wanapokuwa wamemeza dawa za aina yoyote, nguvu ya
dawa inatofautiana kulingana na ugonjwa husika na muda wa kukaa
mwilini,” alisema daktari huyo.
DAKTARI MUHIMBILI ANENA
Ili kuzidi kupata undani
wa mazingira ya kifo cha Kuambiana, Amani lilimtafuta daktari mwingine
mtaalam wa magonjwa ya binadamu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Naye kwa sharti la kutotaja jina alieleza madhara ya mtu kunywa pombe
akiwa kwenye dozi.
“Unapokunywa dawa hususan hiyo fansidar, inakaa katika mwili kwa
takriban siku saba hivyo mgonjwa anapokunywa pombe ndani ya siku hizo,
pombe inapochanganyika na dawa katika mzunguko wa damu hugeuka kuwa sumu
na mgonjwa ana uwezekano wa kupoteza maisha endapo asipowahishwa
hospitalini,” alisema daktari huyo na kuongeza:
“Wengi huwa wanajisahau na kunywa pombe kabla ya siku saba lakini
wengine huwa wanakunywa pombe makusudi pale tu wanapoanza kupata ahueni
ya ugonjwa pasipo kutambua nguvu ya dawa bado ipo mwilini mwake na
madhara yake ndiyo hayo.”
JB AANGUKA GHAFLA, AZUA HOFU
Wakati shughuli za
kuaga mwili zikiendelea juzi, Jumanne katika Viwanja vya Leaders,
Kinondoni jijini Dar, nguli wa filamu nchini ambaye alikatisha ziara
yake ya kikazi nchini Uturuki kwa ajili ya kuja kumzika Kuambiana, Jacob
Steven ‘JB’, alipewa kipaza sauti ili amzungumzie marehemu ambapo akiwa
katikati ya kuongea alianguka ghafla.
Umati wa watu uliokusanyika viwanjani hapo uliingia hofu na kushindwa
kuelewa amepatwa na nini lakini haikuchukua muda mrefu akasaidiwa na
watu na kuendelea na shughuli nyingine.
MASTAA WAONGOZA KWA VILIO
Mastaa mbalimbali wa
Bongo Movies wakiongozwa na Wema Sepetu, Aunt
Ezekiel, Blandina Chagula ‘Johari’, Miriam Jolwa ‘Jini Kabula’
waliongoza kwa kulia viwanjani hapo hadi walipofika makaburini,
Kinondoni.
Mbali na mastaa hao kuangusha vilio, Mkurugenzi wa Aset, Asha Baraka
alijikuta akishindwa kuaga kwa kuhofia kuuona mwili wa marehemu na kudai
huwa akitazama maiti anamuota kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Marehemu Kuambiana ambaye alikuwa nguzo muhimu katika ‘ku-dairekti’
filamu, alipatwa na mauti katika Gesti ya Silvarado, Sinza- Kwaremmy
jijini Dar. Mungu ailaze pema peponi roho ya marehemu. Amina.
Chanzo: Gazeti la Amani/ GPL
Chanzo: Gazeti la Amani/ GPL

