MMOJA wa wasichana wawili raia wa Uingereza waliomwagiwa tindikali na
watu wawili ambao bado hawajajulikana mjini Zanzibar Agosti 7 mwaka
jana, ameibuka na kuliambia gazeti la Daily Mail la nchini humo jinsi
tukio hilo lilivyotokea.
Katika mahojiano yaliyochapishwa na gazeti hilo Jumapili iliyopita,
Katie Gee, ambaye ndiye alikuwa karibu zaidi ya mtu aliyewamwagia
tindikali hiyo, alisema hadi sasa amefanyiwa upasuaji wa ngozi yake mara
15 na kufikia hatua ya kumpa matumaini ya kurejea katika hali yake ya
kawaida.
Katie, ambaye mwili wake uliharibika kiasi cha asilimia 30 kutokana
na tukio hilo, alikuwa na rafiki yake, Kirstie Trup ambao walikwenda
Zanzibar kwa kazi za kujitolea kuwahudumia watoto yatima.
Akizungumzia tukio hilo, msichana huyo anayeishi Hampstead, Kaskazini
ya London, alisema mara tu baada ya kumwagiwa, tindikali hiyo iliondoa
sehemu kubwa ya ngozi yao kuanzia kidevuni hadi tumboni, kiasi cha
kuwafanya waonekane weupe.
“Walikuwa wawili kwenye pikipiki, aliyekuwa amepanda nyuma,
alituangalia na kutabasamu, halafu akachukua dumu na kutumwagia, Kirstie
aliloa mwili mzima.”
Madaktari wanaomtibu wamesema msichana
huyo angeweza kutoona tena kama asingekuwa amefumba macho wakati
alipofanyiwa kitendo hicho.
Kate Gee.
Watu waliokuwa karibu na tukio hilo, waliwasaidia wasichana hao kwa
kuwamwagia maji kuondoa ukali wa tindikali hiyo kabla ya kupelekwa
hospitali, na baadaye kupanda ndege kwenda London kwa matibabu zaidi.
Katie aliharibika ngozi yake usoni, mgongoni, mikononi, tumboni na
miguuni.
Sikio lake moja limelazimika kutolewa baada ya kuharibika vibaya na
madaktari wanafanya mpango wa kumwekea la bandia. Aidha, ili awe mzima
kabisa, anatakiwa kufanyiwa tena upasuaji mara 15 zaidi.
“Zamani nilikuwa naogopa sana kila niliposikia kuhusu upasuaji,
lakini sasa imekuwa ni sehemu ya maisha yangu, madaktari walitaka
kunitoa ngozi yangu ya kichwa ili waiweke sehemu ya uso, lakini
nimekataa kwa sababu kichwa change ndiyo sehemu pekee ambayo haikuguswa
na tindikali,” alisema msichana huyo.
Wasichana hao wawili walimwagiwa tindikali hiyo wakati hali ya
usalama kisiwani Zanzibar ilipochafuka kufuatia matukio mfululizo ya
aina hiyo, kwani mwezi mmoja baadaye, padre mmoja wa kanisa katoliki,
Anselmo Mwang’amba naye alifanyiwa kitendo hicho.
