Na Mwandishi maalumu – HakiElimu
Uchunguzi
kuhusiana na vitabu vilivyonunuliwa kutokana na chenji ya rada na
kusambazwa mashuleni nchini Tanzania umebaini kuwa vitabu hivyo vina
kasoro za ubora licha ya kupata Hati ya Ithibati (Certificate of
Approval) kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Uchunguzi
huo uliofanyika katika shule za msingi katika Wilaya ya Kilwa Masoko
iliyoko mkoani Lindi umebaini pamoja na kasoro za ubora pia mgawanyo wa
vitabu hivyo haukuzingatia mahitaji halisi kwa shule husika. Hii
imesababisha upotevu wa pesa za Watanzania zilizorudishwa nchini baada
ya kuokolewa katika ufisadi wa manunuzi ya rada.
MAPUNGUFU KATIKA VITABU VYA SOMO LA SAYANSI
Mwalimu
mmoja wa somo la Hisabati (jina linahifadhiwa) anayefundisha darasa la
saba ameelezea kupokea vitabu vya kiada vinavyokinzana katika mada
akitolea mfano wa mada ya “Ubongo wa Nyuma,” ambapo kitabu cha
mchapishaji mmoja kikiandika kuwa Serebelamu huhusika na matendo yasiyo ya hiari huku kitabu kingine kikielezea Serebelamu huhusika na uratibu wa matendo ya hiari.
Picha ifuatayo inaonesha mkanganyiko uliopo katika mada ya “Aina za
Misuli” ambapo wachapishaji wanataja majina na aina tofauti za misuli.
MAPUNGUFU KATIKA VITABU VYA SOMO LA KISWAHILI
Akizungumzia
baadhi ya kasoro katika kitabu cha somo lake, mwalimu wa somo la
Kiswahili darasa la sita amesema moja ya kasoro katika kitabu
kilichopokelewa ni kutokuwa na mtiririko maalum wa mada na kuleta
mkanganyiko kwa wanafunzi na walimu. Video ifuatayo inaonesha jinsi mada
ya “Aina za Maneno” ilivyowasilishwa katika kurasa katika ukurasa wa
10, 85 na 118 katika kitabu kimoja, Gonga hapa kuitazama http://bit.ly/1suMuSq
MAPUNGUFU KATIKA SOMO LA HISABATI
Mwalimu wa
Hisabati aliyepata nafasi ya kushiriki katika utafiti huu amezungumzia
kuwepo mazoezi machache sana na mepesi yasiyoweza kumpa mwanafunzi uwezo
wa kutafakari na kupambanua. Vile vile vitabu hivyo vinasemekana
kutokuwa na majibu sahihi ya maswali yaliyotolewa na hivyo kuwapotosha
wanafunzi. Picha ifuatayo inaonesha jibu ambalo halikukotolewa mpaka
mwisho na hivyo kutoa jibu lisilo sahihi katika taaluma ya Hisabati.
MAPUNGUFU KATIKA SOMO LA JOGRAFIA
Katika somo
la Jiografia , baadhi ya makosa yaliyogundulika ni pamoja na kuwepo kwa
taarifa zinazopotosha wanafunzi; mfano katika mada ya “Majira ya Dunia
“katika kitabu kimoja cha kiada kilichonunuliwa kwa chenji ya rada kina
makosa katika tarehe za kupatwa kwa jua
MAPUNGUFU KATIKA MASOMO MENGINE
Kwa upande
wa somo la Historia darasa la saba , Mwalimu amezungumzia uwepo wa
maelezo mafupi sana katika vitabu vya chenji ya rada yasiyotoa elimu
yoyote kwa mwanafunzi anayesoma somo hilo.Alitolea mfano wa mada ndogo
ya kugawanywa kwa wananchi wa Afrika ambayo maelezo yake hayatoi maarifa
yoyote kwa mwanafunzi ikilinganishwa na vitabu vya zamani.
Kwa upande
wa Somo la Kiingereza walimu wamelalamikia ugumu wa lugha iliyotumika
katika vitabu walivyopokea na kusema misamiati mingine huwapiga hata wao
chenga na hakukuwa na sababu ya kutumiwa kwa misamiati hiyo kwa kuwa
lugha ya kawaida ndio msingi wa ufundishaji mashuleni.
MATUMIZI MABAYA YA RASILIMALI ZA UMMA
Utafiti
uliofanywa katika shule nne (4) umegundua kuwa licha ya Serikali kuwa na
takwimu za mahitaji halisi ya vitabu vya shule hizo kulingana na
masomo, mgawanyo wa vitabu vya chenji ya rada bado una mapungufu
makubwa. Masomo ambayo yalikuwa yana upungufu mkubwa wa vitabu bado
yameendelea kutopata kabisa kitabu hata kimoja na au kupokea nakala
chache huku masomo mengine yakipokea vitabu vingi mpaka kupitiliza
mahitaji halisi ya shule husika. Masomo ambayo yameendelea kukabiliwa na
upungufu wa vitabu kwa upande wa Wilaya ya Kilwa ni pamoja na Uraia,
Haiba na Michezo, Stadi za kazi na Historia .
