Na Michael Ngilangwa, Njombe
Mkuu wa mkoa wa Njombe Keptain Mstaafu Aseri Msangi Amewataka wananchi na taasisi za sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika zoezi la upandaji wa miti rafiki kwa vyanzo vya maji na miti ya mbao katika kwa maeneo mengine yanayostahili kupandwa huku akiwatahadharisha na matukio ya moto kichaa na ukataji ovyo.
Aidha Keptain mstaafu Msangi pia amerejea kauli yake ya kuwataka wananchi kupanda miti ya matunda ili iwasaidia kutatua tatizo la kifedha miongoni mwa wananchi na sekta binafsi jambo litakalosaidia kutokatwa kwa miti kabla ya wakati wake ambapo pamoja na mambo mengine wametakiwa kukata mti na kupanda mti kama kauli mbiu ya mwaka huu inavyojieleza.
Akizungumza na wananchi wa mitaa ya Kibena Keptain Msangi amewapongeza wananchi na taasisi binafsi zinazostawisha vitaru vya miche ya miti na kuwataka kutambua umuhimu wa miti hiyo kuwa ni sehemu ya zao huku akiwaagiza viongozi wote wa vijiji na kata kuhakikisha wanalisimamia tatizo la moto kichaa pamoja na wananchi kujitokeza kwa wingi na mapema kuuzimisha moto utakao kuwa umejitokeza maeneo yao.
Hata hivyo amesema kuwa jitihada za kupanda miti zinatakiwa kwenda sambamba na ufugaji wa nyuki katika maeneo hayo huku akiyataka makapuni Na taasisi mbalimbali yaliopo mkoa wa Njombe ikiwemo kampuni ya Tanwat kuhakikisha inaendeleza kupanda maeneo mengine ambayo hayajapandwa miti kwenye vyanzo vya maji.
Katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii bi.Maimuna Tarishi akisoma taarifa ya Wizara ya Maliasili na Utalii amesema kuwa kumekuwapo na ongezeko la upandaji wa miti kwa mwaka 2005 na 2006 hadi 2012 na 2013 takwimu zinaonesha wastani wa miti milioni mia moja sitini na tano kwa mwaka sawa na asilimia sitini na tano ambayo inaendelea kukua mpaka sasa maeneo mbalimbali hapa nchini.
Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Njombe bwana Edwin Mwanzinga amesema kuwa halmashauri ya mji wa Njombe itaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya upandaji na utunzaji wa mazingira hususani kwenye vyanzo vya maji pamoja na matukio ya moto kichaa.
Kwa upande wao wananchi na viongozi wa mitaa ya Kibena wamesema kuwa jitihanda za upandaji miti kwenye vyanzo vya mazingira zimekuwa zikiendelea kila maeneo lakini wanasikitishwa na kampuni ya Tanwat kushindwa kuondoa miti isiyo rafiki kwenye vyanzo vya maji jambo linalosababisha wananchi kukosa maji msimu wa kiangazi kutokana na vyanzo vyake kukauka.
Kauli mbiu ya mwaka Huu inasema Miti ni Uhai Panda miti kwanza Ndipo Ukate Mti ambapo mkoa wa Njombe umepongezwa kwa hatua kubwa ya kupanda miti kwa wingi na kuwataka wananchi na taasisi kuendelea kupanda miti hiyo kwa manufaa yao.