SHERIA inayoruhusu wanaume kuoa mke zaidi ya mmoja, imepitishwa nchini Kenya.
Rais Uhuru Kenyatta ametia saini sheria hiyo licha ya malalamiko kutoka kwa vikundi vya wanawake nchini humo.
Taarifa kutoka katika ofisi ya Rais ilisema kuwa mswada huo ambao unajumuisha vipengee kadhaa kuhusu ndoa , imekuwa sheria sasa.
Mswada huo ulioleta mageuzi katika sheria ya sasa , ulipitishwa na
bunge mwezi jana kuidhinisha rasmi utamaduni wa ndoa ya zaidi ya
mwanamke mmoja.
Taarifa ya Rais ilisema kuwa "ndoa ni muungano wa watu wawili
mwanamke na mwanamume , ikiwa mume atataka kuoa mke mmoja au wawili,
mwenyewe anapaswa kuamua.''
Mswada wa awali, ulimpa mwanamke haki ya kwenda mahakamani kupinga
mume wake kuoa mke wa pili, lakini wabunge wanaume waliungana katika
kuunga mkono mswada huo.
Wakati mswada huo ulipopitishwa mwezi jana, wabunge wanawake waliondoka bungeni kwa hasira baada ya mjadala mkali.
Shirikisho la kitaifa la mawakili wanawake pia limesema kuwa litapinga sheria hiyo mahakamani.
Katika sehemu nyingi barani Afrika, kuoa zaidi ya mwanamke mmoja ni
jambo la kawaida katika tamaduni nyingi sawa na hali ilivyo nchini Kenya
na hata pia miongoni mwa waumini wa dini ya kiisilamu.
Wengi wanasema kuwa sheria hiyo inapiga tu muhuri wa utamaduni uliopo.
Chanzo: BBC SWAHILI
