ASKARI Polisi wanne wa kituo cha Polisi Singida mjini na wakazi 15 wa kijiji cha Utaho tarafa ya Ihanja wilaya ya Ikungi mkoani Singida,wamefariki dunia baada ya kugongwa na basi la kampuni ya summry T.799 BET aina ya nissan.
Tukio hilo limetokea Aprili
28 mwaka huu saa 2.45 usiku katika barabara kuu Singida-Dodoma eneo la
kijiji cha Utaho wilaya ya Ikungi.
Kwa mujibu wa Kamanda wa
Polisi mkoa wa Singida,SACP.Geofrey Kamwela askari hao ni F.849 D/CPL
Boniface Magubika,F.6837 Pc Jumanne Mwakihamba,G.7993 Pc Novatus Tarimo
na G.8948 Pc Michael Mwakihaba.
Alitaja wengine waliofariki
kuwa ni pamoja na Ramadhani Mjengi afisa mtendaji wa kijiji cha
Utaho,Paul Hamisi mwenyekiti wa kijiji cha Utaho,Ernest
Salanga,mwenyekiti wa kitongoji cha Utaho,Saidi Rajabu,Usirika
Itambu,Chima Mughenyi,Slim Juma,Abeid Ramadhani,Mwinyi Hamisi na Issa
Husein wote wakazi wa kijiji cha Utaho.
Aidha,Kamwela amesema kuwa
miili ya watu wengine bado haijatambuliwa na imehifadhiwa kwenye chumba
cha maiti cha hospitali ya mkoa mjini Singida.
Akizungumuzia juu ya ajali
hiyo,kamanda huyo amesema kuwa awali kijana Gerard Zephania (24) akiwa
ametoka kusaga nafaka aligongwa na gari la mizigo ambalo bado
halijafahamika na kufariki papo hapo.
“Askari wa polisi wakitumia
gari PT 1424,walifika eneo la tukio kwa ajili ya kuubeba mwili wa
Gerard kuuleta katika hospitali ya mkoa kwa uchunguzi,kundi la wananchi
wa kijiji cha Utaho nao walifika eneo la tukio”,amesema na kuongeza;
“Wakati askari polisi
wakiwa kwenye harakati ya kuupakia mwili huo ghafla basi la summry
liliacha njia na kuingia kushoto mwa barabara kwa nia ya kulikwepa gari
la polisi na ndipo lilipovamia na kugonga kundi la watu hao wakiwemo
askari polisi.Watu 15 walifariki papo hapo”,amesema Kamwela.
Kamanda Kamwela amesema
kuwa dereva wa basi hilo Paulo Njilo mkazi wa Dar-es-salaam hakuweza
kusimamisha basi hilo nadi kilomota 25 alipolisimamisha na yeye
kutorokea kusikojulikana.
Aidha,amesema ajali hiyo
imesababisha majeruhi nane ambapo wawili kati yao wamelazwa katika
hospitali ya mkoa na hali zao zinaendelea vizuri.Majeruhi wengine sita
wamelazwa katika hospitali ya misioni ya Puma na hali zao sio nzuri.
“Uchunguzi zaidi juu ya
ajali hiyo unaendelea ili kujua chanzo halisi cha tukio pamoja na
kumtafuta dereva wa basi ili aweze kuhojiwa na kisha hatua za kisheria
ziweze kuchukuliwa dhidi yake”,amesema Kamanda Kamwela.
