WAGANGA WATOKOMEA KUSIKOJULIKANA BAADA YA KUWATAPELI WATU MAKETE MJINI

Sakata la kuibuka kwa rundo waganga wa jadi wilayani Makete mkoani Njombe limechukua sura mpya baada ya baadhi yao kuwatapeli wananchi na kutokomea kusikojulikana na kuacha majonzi kwa wananchi hao. 

Hatua hiyo inafuatia ofisi ya Mganga mkuu wilaya ya Makete kwa kushirikiana na wananchi na waandishi wa habari wilayani hapo kuibua taarifa hizo ambapo imebainika baada ya waganga hao kutua makete mjini wamekuwa wakiendesha shughuli zao bila kibali wala kutoa taarifa jambo ambalo ni kinyume cha sheria. 

Akizungumza na mwandishi wa mtandao huu Afisa afya wa wilaya ya Makete Bw. Boniphace Sanga amesema ni kinyume cha sheria kwa waganga kufanya kazi zao bila kibali cha serikali pamoja na kutoa taarifa kwa viongozi husika wa eneo analofanyia shughuli zake. 

Amesema suala la waganga hao kujiita waganga wa jadi ni makosa na badala yake wanaitwa wataalamu wa tiba mbadala na pia kitendo cha kubandika matangazo yao wenye nguzo za umeme ni makosa pia. 

Bw. Sanga amesema baada ya ofisi ya mganga mkuu wa wilaya kupata taarifa za waganga hao kuingia wilayani hapo na kufanya shughuli zao kienyeji wameamua kuchukua hatua ya kuwafikia waganga hao ili kuwataka wawape kibali kinachowaruhusu kufanya hivyo na alipofika katika nyumba moja hakuwakuta wahusika ambapo alivikuta baadhi ya vitendea kazi ambavyo alivitilia shaka na alipoondoka kwenda kuwaita waandishi wa habari ili kufika kujionea hali halisi hawakuvikuta na walishangaa kukuta nyumba hiyo imefungwa na waganga hao kutokomea kusikojulikana. 

Ametoa wito kwa wananchi kuwa makini kwa kuwa watu hao ni matapeli ambapo kwa habari ambazo hazijathibitishwa kwa asilimia 100 wapo baadhi ya wananchi wametapeliwa fedha kwa kuahidiwa kuwa wangesafishwa nyota ambapo mwandishi wetu alimshuhudia mama mmoja (jina tunalihifadhi) akilia kwa uchungu mara baada ya kukuta mganga aliyemuahidi kumsafishia nyota ametoweka katika mazingira ya kutatanisha. 

Mwandishi wetu alifika kituo cha polisi Makete na kuzungumza na Mkuu wa polisi wilaya ya Makete Bw. Alfred Kasonde ambaye amesema yeye hana taarifa za kuwepo waganga hao ambao pia walitakiwa kutoa taarifa kwake kabla ya kuanza kazi na kuahidi kulifuatilia mara moja. 

Hivi karibuni zilizipotiwa taarifa za kuweo kwa waganga wa jadi waliovamia Makete mjini na kubandika vibao kwenye nguzo za umeme kujinadi kuwa wanatibu magonjwa mbalimbali bila kuwa na kibali, jambo lililovaliwa njuga na viongozi mbalimbali na ndipo matapeli hao walipoamua kukimbia kukwepa mkono wa sheria. 

Na Edwin Moshi wa EDDY BLOG


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo