Mratibu wa Idara ya Maafa
kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bwana Harrison Christopher Chinyuka
Chinyuka, akiendesha mafunzo kwa waandishi na watangazaji wa Redio za
Jamii nchini.
Na Mwandishi Wetu
Ukosefu wa taarifa na lugha sahihi halikadhalika kukosa uelewa katika
jamii ni miongoni mwa mambo yanayosababisha kutokea kwa maafa.
Katika mada inayohusu Misaada ya Kibinadamu na Taarifa za Maafa
katika mafunzo ya siku nne ya wanahabari na watangazaji wa redio jamii
mjini Kahama Mratibu wa idara ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bwana
Harrison Christopher Chinyuka alisema jamii lazima ifahamu historia ya
maeneo yanapotokea maafa na wapate elimu ya kutosha ili waweze kuepusha
maafa asili.
Bwana Chinyuka alisema kwamba hilo litafanikiwa iwapo waandishi wa
habari watawajibika kikamilifu kwa kuandika taarifa za majanga na maafa
ambazo ni sahihi na kwa wakati kwa sababu wakati mwingine wamekuwa
wakishindwa kutumia lugha sahihi ya kusheheneza taarifa husika.
“Wanahabari wana mchango mkubwa katika kuhakikisha kuwa madhara ya
maafa yanapunguzwa kwa kuipa uelewa jamii husika kwa kutoa taarifa na
lugha sahihi zinazohusu maafa ili kutoa nafasi kwa wahanga kujihami
ipasavyo”, alisema Bwana Chinyuka.
Wajibu wa mwandishi wa habari katika kupunguza maafa ni kukuza uelewa
wa jamii kuhusu hatua za hatari, kuzuia na kukabiliana na maafa,
kukubaliana juu ya viwango vya taratibu za uendeshaji katika sehemu ya
maafa.
Wajibu mwingine ni kusambaza ujumbe wa onyo kwa kuaminika na haraka
iwezekanavyo na kuiweka jamii vizuri kitaarifa wakati huo huo kuepuka
uvumi na hofu katika hali ya hadhari.
“Wajibu wenu waandishi wa habari kabla, wakati na baada ya maafa ni
kutimiza jukumu la kulinda na kusaidia kuunganisha familia na kujenga
kujiamini, sio kuachia mchakato njiani”, alisema Bwana Chinyuka.
Madhumuni ya mafunzo hayo ni kutoa uwezo kwa waandishi wa habari na
watangazaji wa redio jamii kuandika taarifa zinazohusu kutoa msaada wa
kibinadamu na kupunguza madhara yatokanayo na majanga na maafa nchini
katika mradi unofadhiliwa na shirika la maendeleo ya Sweden (SIDA) kwa
kushirikiana na UNESCO.
Mafunzo hayo yanatekeleza malengo ya UNESCO linalohusisha kuimarisha
uwezo wa kukuza mazingira ya uhuru wa kujieleza kwa ajili ya maendeleo,
kuendeleza demokrasia na utamaduni wa mazungumzo ya amani bila migogoro.
